Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, amezindua kampeni ya “Ongea na Kamanda” katika Soko la Nyamkazi, Kata ya Miembeni, Manispaa ya Bukoba, kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi Ili kubaini changamoto za kiusalama na kuzitafutia ufumbuzi.

Wananchi wa kata hiyo wameipokea vyema kampeni hiyo wakieleza kuwa inawapa fursa ya kuwasilisha moja kwa moja changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa kero zilizotajwa ni wizi wa mbuzi, ambao wamesema umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo yao kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo.
Kwa upande mwingine, wavuvi wa dagaa wa Nyamkazi na maeneo jirani wamelalamikia kutozwa faini kwa kuingia katika maeneo ya hifadhi, wakieleza kuwa wanatakiwa kufanya shughuli zao ndani ya umbali wa kilomita mbili bila kuvuka eneo lililoruhusiwa. Wamesema kutokuwepo kwa alama zinazoonesha mipaka hiyo ziwani kunafanya iwe vigumu kwao kutambua eneo sahihi la kufanyia shughuli za uvuvi.

Aidha, Shamimu Seif ameeleza changamoto wanayokutana nayo wananchi wanapohitaji msaada wa migambo kwenda kuwakamata watuhumiwa, akidai kuwa baadhi yao huwatoza fedha bila kuwa na kiwango maalumu. Amesema hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo katika kushughulikia changamoto zao za kiusalama.

Akijibu kero hizo, Kamanda Chatanda amekemea kitendo cha baadhi ya migambo kudai fedha kutoka kwa wananchi ili kwenda kuwakamata watuhumiwa na kusema kuwa maelekezo ya kutotumia migambo katika vituo vya polisi tayari yametolewa, huku akipiga marufuku uwepo wao katika vituo hivyo lakini pia ameahidi kufanyia kazi suala la wizi wa mifugo.

Hata hivyo, Kamanda Chatanda amesema kero zote zilizowasilishwa kupitia kampeni hiyo ataziwasilisha katika mamlaka husika ili zichukuliwe hatua na kupatiwa ufumbuzi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya polisi na wananchi katika kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Discussion
Reader comments
0 contributions