Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Gerald Mongella amesema nyuki ni viumbe muhimu wenye mchango mkubwa katika maisha ya binadamu, mazingira pamoja na uchumi kupitia shughuli za uchavushaji wa mazao na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyuki.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha leo Mei 20, 2026 wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika katika Chuo cha Ufugaji Nyuki kilichopo katika Manispaa ya Tabora, Dkt. Mongella amesema nyuki wanastahili kuthaminiwa kutokana na nafasi yao kubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

“Ukimtazama mdudu nyuki anastahili kabisa kutengewa siku yake. Kupitia uchavushaji, nyuki wanachangia upatikanaji wa chakula kwa binadamu na pia wana mchango mkubwa katika utunzaji wa ikolojia na mazingira,” amesema Dkt. Mongella.
Katika hotuba yake, DC Mongella ametaja changamoto zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na uharibifu wa misitu na uchomaji wa miti, hali inayotishia makazi ya nyuki na kuathiri mazingira.

Amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizo ili kuhakikisha sekta ya nyuki inaendelea kuwa na tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia amekitaka Chuo cha Ufugaji Nyuki kuendelea kutoa elimu kuhusu thamani ya mazao mbalimbali yatokanayo na nyuki, akieleza kuwa asali siyo zao pekee lenye manufaa kwani zipo bidhaa nyingine nyingi zenye thamani kubwa kiuchumi.

Katika kuonesha kuunga mkono juhudi za uhifadhi na ufugaji nyuki, DC Dkt. Mongella ametundika mzinga wa nyuki, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa maadhimisho hayo.
Discussion
Reader comments
0 contributions