Na Saada Almasi, Busega - Simiyu.
Wakazi wa kitongoji cha Nyuma ya Mlima ambacho kinapakana na pori la akiba Kijereshi wilayani Busega mkoani Simiyu wamelazimika kuchanga fedha na kufanikisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu ili kuwalinda watoto wa chekechea dhidi ya wanyama wakali kama fisi wanaotokea katika pori hilo ambao wamekuwa wakiwavamia watoto hao pindi wanapotoka ama kwenda shule.
Awali, watoto hao walilazimika kufuata elimu umbali wa kilometa 8 katika shule ya msingi Nyamikoma wamekuwa wakikumbana na mikasa ya uvamizi wa wanyama hao na wakati mwingine wakikutana na tembo maeneo ambayo hakuna makazi ya watu na hivyo kukosa mtu wa kuwasaidia.

Wakiwa katika kikao cha pamoja wananchi hao wamesema kuwa kila ambapo mototo aliondoka kuelekea shuleni wazazi walibaki na wasiwasi hali iliyopelekea baadhi yao kuwasitishia masomo watoto wao.
“mwanzo tulichanga elfu 25 kila mmoja tukafanikiwa kununua eneo la ekari 11 kwa shilingi milioni 5 na baadae tukachanga shilingi elfu 15 ili tuanze kunyanyua boma,tumefanya kwa kujitoa sana ili watoto wetu waendelee kupata masomo maana kule walikokuwa wanaenda walikuwa wanakumbwa na matukio mengi ya wanyama wakali,” alisema Mkazi wa kitongoji cha Nyuma ya Mlima, Mariam Jota.

“tumelazimika kuwakatisha watoto shule baadhi yetu maana huko Nyamikoma ni umbali wa kilometa 8 sasa fikiria mototo wa chekechea kutembea hadi umbali huo kwenda na kurudi kwa siku,bado hapa njiani hajakutana na wanyama wakali kama mzazi unalazimika kuchukua maamuzi magumu” alifafanua mkazi wa Nyuma ya Mlima, Saguda Shawishi.
Wamesema, kando na hofu kwa watoto wadogo bado hata watu wazima wamekuwa wakipata wakati mgumu kupita maeneo ya karibu na pori hilo kwani wanyama kama tembo imekuwa kawaida kukutana nao.

Jitihada za wakazi hao ambazo zilifikisha kiasi cha shilingi miloni 3 na laki nne zimenyanyua vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu hatua ambayo imeigusa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambao wamechangia mabati 60 ambayo yanakwenda kutumika katika kufunika jengo hilo.
“tumeona jitihada zenu na kwa kuwa mlifika kwetu na kutuomba tuwashike mkono leo hii tunawapatia mabati 60 ambayo mtayatumia kuezeka vyumba hivi ,kingine niwapongeze juhudi zenu ni kubwa mno eneo la ekari 11 mlilonunuakwa michango yenu bila kushurutishwa linauwezo wa kuzalisha shule nyingine wakaweza kusoma watoto wengi zaidi na hii ndiyo tafsiri halisi ya umoja ni nguvu,” alisema Floravick Kallambo.

Mamlaka hiyo pia imetoa wito kwa wakazi wa maeneo karibu na pori hilo kuhakikisha wanashiriki katika uhifadhi wa pori hilo na kuacha mara moja shughuli za kuchumi ndani ya pori ambazo kwa kiasi kikubwa zinahatarisha maisha ya wanyama.
Discussion
Reader comments
0 contributions