Skip to main content

NGS YAONGEZA THAMANI MAZAO YA WAKULIMA WA PAMBA KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

NGS YAONGEZA THAMANI MAZAO YA WAKULIMA WA PAMBA KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Kiwanda cha uchakataji wa pamba cha NGS kilichopo Kijiji cha Ifukutwa, Kata ya Mpanda Ndogo, Wilaya ya Tanganyika, kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Katavi kwa kuongeza thamani ya zao la pamba, kutoa ajira na kufungua fursa mpya za uwekezaji.

Hayo yamebainika wakati wataalamu kutoka Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi walipofanya ziara ya mafunzo kiwandani hapo, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na uchakataji wa pamba pamoja na kutathmini fursa zilizopo katika sekta ya viwanda na uwekezaji mkoani humo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kiongozi wa Msafara ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Florence Chrisant, alisema kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Katavi.

Amesema kiwanda hicho kimezalisha ajira zaidi ya 300 za kudumu na za muda kwa Watanzania, huku kikiongeza thamani ya zao la pamba na kuboresha kipato cha wakulima kupitia soko la uhakika la mazao yao.

"Kiwanda hiki kinaonyesha kwa vitendo jinsi uwekezaji katika sekta ya viwanda unavyoweza kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, kukuza uchumi wa eneo husika na kutoa ajira kwa wananchi wengi," alisema Bw. Chrisant.

Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi una fursa nyingi za uwekezaji, hususan katika viwanda vya vifungashio, nguo na usindikaji wa mazao ya kilimo, kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika kutoka Gridi ya Taifa pamoja na eneo la ekari 576.5 lililotengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji.

Alieleza kuwa mazingira hayo yanaifanya Katavi kuwa eneo lenye mvuto kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya kisasa, akiongeza kuwa upatikanaji wa malighafi za kutosha pamoja na maeneo makubwa ya uwekezaji ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuharakisha maendeleo ya viwanda na uchumi wa mkoa huo.

Bw. Chrisant ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo Katavi kwa kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuzalisha ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Tunawaalika wawekezaji kuja Katavi kwa sababu mazingira yaliyopo yanawezesha uwekezaji wenye tija na wenye manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla," amesisitiza.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.