Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Ndege ya majaribio imefanikiwa kutua na kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Shinyanga uliopo Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza kwa huduma rasmi za usafiri wa anga kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani.
Akizungumza kwenye hafla ya kushuhudia tukio hilo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa asilimia 100 ifikapo Septemba 1, 2026, ili kutoa huduma xa usafiri wa anga.

Prof. Mbarawa amesema, kwasasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 98 na kwamba anaufahamu mradi huo tangu ulipoanza kutekelezwa alipokuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akisisitiza kuwa ni lazima ukamilike kwa wakati ili huduma za anga zianze kunufaisha wananchi wa Shinyanga.
Amesema viwanja vya ndege vya Tabora, Sumbawanga na Kigoma tayari vimekamilika, hivyo hakuna sababu ya Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuchelewa kukamilika.

Aidha, amesema ujenzi wa uwanja huo pamoja na miradi mingine ya viwanja vya ndege nchini unalenga kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga, kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji pamoja na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kukamilika kwa uwanja huo kutakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa mkoa kwa kuwezesha usafiri wa haraka wa watu na mizigo pamoja na kuvutia wawekezaji.

Naye Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Mhandisi Japherson Nnko, amesema mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga ulianza Aprili 2023 na ulipitia changamoto zilizochelewesha utekelezaji wake kwa muda.
Amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 45 sasa umefikia unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2026, tayari kwa kuanza kutoa huduma za ndege za abiria kuanzia Septemba 1 mwaka huu.

Usafiri wa anga ni mojawapo ya njia muhimu za usafiri duniani. Faida yake kubwa ni kasi, kwani huwezesha watu na mizigo kufika maeneo ya mbali kwa muda mfupi sana. Hali hii huokoa muda na kuongeza ufanisi katika shughuli za kibiashara na kijamii.
Pia, usafiri wa anga huchangia kukuza uchumi kwa kurahisisha biashara, utalii na uwekezaji kati ya nchi mbalimbali. Aidha, hutumika katika kutoa huduma za dharura kama vile kusafirisha wagonjwa, dawa na misaada wakati wa majanga.

Kwa ujumla, usafiri wa anga una mchango mkubwa katika kuunganisha watu, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kurahisisha mawasiliano duniani.



Discussion
Reader comments
0 contributions