Skip to main content

NANAUKA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUONGEZA UWAJIBIKAJI, VIJANA WAPEWA KIPAUMBELE FURSA ZA ZABUNI

Na Daniel Gahu - Katavi.

NANAUKA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUONGEZA UWAJIBIKAJI, VIJANA WAPEWA KIPAUMBELE  FURSA ZA ZABUNI

Na Daniel Gahu - Katavi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka watumishi wa umma mkoani Katavi kuongeza uwajibikaji, weledi na kasi katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma za umma.

Akizungumza katika kikao chake na watumishi wa umma pamoja na wakuu wa idara mbalimbali mkoani humo, Nanauka amesema kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Amesema, malalamiko mengi yanayowasilishwa na wananchi, hususan vijana, yanaweza kutatuliwa katika ngazi za idara na taasisi za serikali bila kusubiri yafike kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mnayo mamlaka na uwezo wa kuyatatua mengi ya malalamiko ya wananchi kabla hayajamfikia Mheshimiwa Rais. Ni muhimu kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu na uwajibikaji," amesema Nanauka.

Katika hatua nyingine, akiwa ametembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya kilichopo mkoani Katavi, Waziri Nanauka amesema serikali kupitia wizara yake inaendelea kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Amesema kwa sasa wizara yake imeamua kutoa kipaumbele kwa vijana katika zabuni mbalimbali za ofisi, zikiwemo huduma za chakula, usafi, mapambo na huduma nyingine, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kiuchumi na kupunguza malalamiko kuhusu ukosefu wa fursa.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa taifa sambamba na kutekeleza dhamira ya serikali ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kukuza vipato vyao.

Joel Nanauka yupo katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Katavi, yenye lengo la kusikiliza, kufuatilia na kutatua changamoto zinazowakabili vijana katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Ziara hiyo inafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, "Punguza Itifaki, Tukutane Site," ikiwa ni mkakati wa kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza maoni yao na kutafuta suluhisho la changamoto zao kwa wakati.

Serikali inaendelea kusisitiza uwajibikaji wa watumishi wa umma pamoja na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga taifa lenye huduma bora na fursa sawa kwa wananchi wote.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.