Skip to main content

NANAUKA AWATAKA VIJANA KUZINGATIA MAADILI, AWEKA JIWE LA MSINGI BWENI LA WAVULANA KABUNGU

Na Daniel Gahu - Katavi.

NANAUKA AWATAKA VIJANA KUZINGATIA MAADILI, AWEKA JIWE LA MSINGI BWENI LA WAVULANA KABUNGU

Na Daniel Gahu - Katavi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Kabungu, iliyopo Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza fursa za elimu kwa vijana nchini.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Nanauka amewataka vijana na wanafunzi nchini kuzingatia maadili mema, nidhamu na unyenyekevu, akieleza kuwa sifa hizo ndizo msingi wa mafanikio katika maisha na uongozi.

Waziri Nanauka amesema nafasi aliyonayo leo serikalini ni matokeo ya kujenga tabia njema, kuwaheshimu wengine na kufanya kazi kwa bidii, huku akisisitiza kuwa kila kijana ana nafasi ya kufikia ndoto zake endapo ataweka mbele maadili na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu mustakabali wake.

Amesema, "Hata nafasi niliyonayo leo ni matokeo ya kuwa na tabia njema na unyenyekevu. Nawasihi vijana wote muzingatie maadili mema ili siku moja nanyi muweze kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kulitumikia taifa."

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewakumbusha vijana umuhimu wa kuilinda na kuitunza amani na utulivu uliopo nchini, akieleza kuwa maendeleo ya elimu, uchumi na ustawi wa jamii hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira salama na yenye utulivu.

Amesema vijana wanapaswa kuepuka kushawishika kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa, badala yake washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kujenga taifa lenye umoja na ustawi.

Wakati huo huo, akiwa katika ziara yake mkoani Katavi, Nanauka ametembelea na kukagua shughuli za kikundi cha vijana cha JOSA International Supply Group, kilichonufaika na mkopo unaotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Kupitia mkopo huo, kikundi hicho kimefanikiwa kuanzisha duka la uuzaji na usambazaji wa vifaa vya umeme ndani ya Wilaya ya Tanganyika, hatua ambayo imeongeza fursa za ajira, kipato na ushiriki wa vijana katika shughuli za kiuchumi.

Waziri Nanauka amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikopo ya vijana ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya katika kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Ziara ya Mheshimiwa Nanauka katika Mkoa wa Katavi inaendelea kwa lengo la kusikiliza maoni na changamoto za vijana, kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na vikundi vya vijana pamoja na kutathmini namna ambavyo programu za uwezeshaji wa kiuchumi zinavyotekelezwa.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa vijana kupitia elimu, ujuzi, mitaji na fursa mbalimbali za kiuchumi, kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea na kuwa nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya Taifa.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.