Na Saulo Stephen - Singida.
Watumishi wa umma wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, haki na uzalendo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki katika maeneo yao.
Wito huo ametolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Naima Chondo wakati wa ufunguzi wa zoezi la utoaji wa elimu ya uraia, utawala bora pamoja na usimamizi wa mali na rasilimali asilia za nchi kwa viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo Mafunzo hayo yameandaliwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Katiba na Sheria yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Bi. Chondo amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa nafasi walizonazo ni dhamana kubwa kutoka serikalini na kwa wananchi, hivyo wanapaswa kuzitumia kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, usawa na uaminifu katika utoaji wa huduma.
“Sisi kama wawakilishi wa serikali katika kuwatumikia wananchi, kila eneo na kila uamuzi tunaoufanya una athari katika maisha ya wananchi, hivyo yatupasa tufanye kazi kwa umakini na uadilifu. Ni imani ya Serikali yetu kuwa kila mtumishi atatumikia wananchi kwa haki bila ubaguzi na kwa moyo wa uzalendo,” amesema Naima.

Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo viongozi na watendaji katika kuimarisha utawala bora, usimamizi wa rasilimali za taifa pamoja na kukuza uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Sanjari na hayo amewapongeza wawezeshaji kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutoa elimu hiyo muhimu, akieleza kuwa mafunzo hayo yataongeza maarifa na ufanisi kwa viongozi na watendaji katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Discussion
Reader comments
0 contributions