Na Saulo Stephen - Singida.
Baraza la UVCCM Mkoa wa Singida limeazimia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendelea kuifungua Tanzania kidiplomasia na kuimarisha mahusiano ya kimataifa, hatua ambazo zimeendelea kuongeza ushirikiano wa maendeleo, uwekezaji na nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
Azimio hilo limepitishwa katika kikao cha kikanuni cha Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Singida kilichoongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Zulfat Ally Muja, pamoja na Katibu wake Benedicto Bujiku, huku kikihudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Mkoa na wajumbe wa Baraza hilo pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Singida, Eliphas Lwanji, aliyemwakilisha Katibu wa Mkoa.
Katika kikao hicho, Mbunge wa Viti Maalum Kundi la Vijana Taifa, Timida Mpoki Fyandomo, akimuwakilisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Baraza Hilo.

Akizungumza mbele ya wajumbe, aliwapongeza viongozi na wanachama wa UVCCM kwa juhudi wanazoendelea kufanya katika kuimarisha chama, jumuiya pamoja na kuanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ya kiuchumi inayochochea maendeleo ya vijana. Huku akiwapongeza kwa Baraza zuri.
Baraza hilo limeeleza kuwa hatua za Rais Samia za kufanya ziara za kimkakati katika mataifa mbalimbali duniani zimeongeza ushirikiano wa kidiplomasia na kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na mataifa rafiki.
Hali hiyo imeendelea kuvutia wageni mashuhuri, wawekezaji, taasisi za kimataifa pamoja na viongozi kutoka nchi mbalimbali kutembelea Tanzania kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.

Aidha, wajumbe wa Baraza hilo wameazimia kumpongeza na kumuunga mkono Rais Samia kwa namna anavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Baraza limebainisha kuwa utekelezaji huo umeendelea kuleta maboresho katika huduma za kijamii, miundombinu, elimu, afya na mazingira bora ya uwekezaji, jambo linalochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Sambamba na hilo, Baraza limepongeza juhudi za Rais Samia katika kusimamia ukuaji wa uchumi wa Taifa pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi. Wajumbe wameeleza kuwa ukuaji wa uwekezaji wa ndani na nje umeendelea kuchochea ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha shughuli za maendeleo.
Pia wameonesha imani yao katika uongozi wake wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani, utulivu na mshikamano.
Discussion
Reader comments
0 contributions