Watu wasiopungua 25, wameuawa na wengine 22 kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila, yaliyotokea katika eneo la mpakani kati ya mikoa ya magharibi ya Chad ya Hadjer-Lamis na Barh el Gazel.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa Wizara ya Tawala za Mitaa na Ugatuaji Madaraka ilisema mapigano hayo yalihusisha jamii mbili "ndugu".
Jumla ya watu 39 waliokamatwa kuhusiana na ghasia hizo wamepelekwa katika mji mkuu, N'Djamena, kwa hatua zaidi za kisheria.

Serikali Nchini humo, ilituma ujumbe ulioongozwa na Waziri wa Usalama wa Umma na Uhamiaji Ali Ahmat Aghabach kwenda eneo lililoathirika kushughulikia hali hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Mamlaka zilisema zitafanya uchunguzi wa kina kuhusu ghasia hizo, kubaini wahusika na kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuata mkondo wake.
Pia zimeahidi kuongeza nguvu ya mazungumzo kati ya jamii hizo ili kurejesha amani na kuzuia kuongezeka zaidi kwa ghasia.
Mapigano ya kikabila, ni jambo la kawaida nchini Chad na mara nyingi huchochewa na migogoro ya kugombea rasilimali kama vile maji na ardhi.
Discussion
Reader comments
0 contributions