Na Sada Almasi, Mwabayanda, Busega – Simiyu.
Katika kata ya Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu kipo kijiji maarufu cha Mwabayanda ukifika hapa unakutana na kitongoji cha mzee Fabian Masingi wenye umri wa miaka 77 ambaye kuanzia ujana wake hadi sasa amebarikiwa kuoa wanawake 15 ambao tayari wamemzalia watoto 66 pamoja na wajukuu 184 na vitukuu 7.
Familia hii ambayo inaishi kwa umoja na upendo ipo katika kitongoji kimoja wakitofautiana nyumba za kulala japokuwa wamekuwa wakiingiliana bila ubaguzi miuongoni mwao hasa kwa watoto na wajukuu huku wakilelewa na mama hao ambao wanawalea kwa usawa.
Mzee Fabian ameiambia Jambo FM kuwa kitu pekee ambacho anajivunia na familia yake ni upendo ambao ameutengeneza kutoka kwake kuja wa wakeze ambao na hatimaye kwa watoto na kutokana na hilo bado ataendelea kuzaa hadi pale Mungu atakapomnyima uwezo huo.

“Nimeoa nikiwa na miaka 29 mke wa kwanza akiwa na miaka 20,lakini baadae niliendelea kuoa hadi sasa nimefikisha wake hawa 15,hawa wanawake wametaka wenyewe kuolewa na mimi sikuwalazimisha niliomba ridhaa wakakubali, ninawatunza wote bila ubaguzi kwa kadiri ninavyo jaaliwa japo kuna kipindi kigumu lakini natimiza majukumu yangu na nitaendelea kuzaa kwa sababu wako wengine ni wadogo hivyo nitazaa watoto tu maana tuliambiwa tuijaze dunia,” alibqinisha Mzee Fabian Masingi.
“Ninategemea kilimo ambacho awali nilianza kulima katika shamba la Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere huko Butiama ambaye alinifunza mengi ikiwemo kuishi kwa ujamaa na upendo na ndiyo maana hii familia nimeiweka pamoja upendo umetawala,hadi sasa ninalima japokuwa umri unaenda ila sijachoka kiasi cha kuacha kilimo pamoja na watoto wangu”mzee Masingi.
Anasema, ”nimelima kwenye nyakati ngumu sana nakumbukia nilikuwa ninakaa shambani siku 61 bila kurudi nyumbani siku moja nilizimia shambani kwa sababu ya njaa,mke wangu wa tatu ndiye aliyenisaidia baada ya kuja kuniletea chakula na kunikuta pale chini,nilijua mimi ndiye wa kulisha familia lazima nifanye kazi."

Wake wa mzee huyo wanajivunia kuolewa naye wakidai kuwa mzee Fabian ni mtu wa pekee ambaye ametawaliwa na upendo na kujali wake zake.
“Nimezaliwa 2003 nikiwa na miaka 15 mzee alikuja kuniposa na wakati mzee huyu amekuja mimi mwenyewe nilikubali na nilijua ana wake wengine 14 nikataka niwe mke wa 15 kwa sababu huko kijijini kila mtu anajua sifa zake za kujali wanawake ,na tangu nimefika hapa sijawahi kupata shida nikiwa nae na hata nilio wakuta wamenipokea vizuri” Kabula Masunga mke wa 15 wa mzee Masingi.
“Wakati amekuja kwetu na kuongea za wazazi wangu mimi niliitwa na akaniambia tayari ana wake 10 yaani mimi niwe wa 11,wazazi waliponiuliza maoni yangu niliwaambia nataka kuolewa nae nikaolewa ,baadae alipotaka kuongeza mke mwingine niliacha aongeze kwa sababu hata mimi niliwakuta na tunaishi vizuri,” huyu ni Minga Ngelendo mke wa 11 wa mzee Masingi
Pamoja na falimia kuwa kubwa suala la elimu hakuliacha na kusisitiza watoto na wajukuu zake kusoma kwani elimu haina mwisho.

“Mimi sikusoma kabisa lakini watoto wetu na wajukuu lazima kwenda shule tunawahimiza huko bila kuwabagua na hatumlazimishi mtoto aoe mapema ye mwenyewe ataamua atakapokuwa tayari,na wapo kati yao wengine wamepata ajira serikalini kwa sababu wamesoma na linapofika suala la kuwakemea huwa tunawaelekeza wote kwa usawa siyo mtoto wangu tu bali mtoto wa mwingine akikosea namchukua kama wangu” anabainisha Anna Kasasali mke wa tatu.
Watoto wa mzee Fabian wanamchukulia baba yao kama mfano katika maisha yao akiwaonyesha njia sahihi ya kuishi na watu pamoja na familia zao kwa upendo na kuendelea kuzipambania.
“Nakumbuka miaka ya 90 baba alilima shamba lake lakini hakupata mavuno yote yaliharibika lakini hakukata tamaa alituchukua wote na mama zangu tukaenda kulima upya tukapanda baada ya siku chache ikaja mvua kubwa tukapata mazao mengi,nilipata somo kubwa sasa la kutokata tamaa na hata katika masomo kila aliponiambia nioe nilimwambia baba acha nisome,leo hii nimekuwa mwalimu na kupitia mimi amepata nguvu za kusomesha wadodo zangu vile wanataka,” qnqbqinisha Emmanuel Masingi Mtoto wa kwanza wa kiume.
“Mimi ni yatima Mama yangu alifariki muda mrefu nimebaki nikilelewa na mama zangu wa kambo kwa kweli wameniondoa ukiwa sijihisi kama sina mama,wao ndiyo mama zangu ,hadi nafika muda wa kuolewa wamenipa melezi mazuri,sijui neno gani litakuwa zuri kwao ninawashukuru sana,” anasema Felister Masingi mtoto wa kwanza wa kike.
Kitu pekee ambacho mzee Fabian anikitamani ni serikali kumtambua na kumsaidia kupata trekta kwa ajili ya shughuli zake za kilimo kwani ndiyo kitega uchumi ambacho anakitegemea katika maisha yake.
Discussion
Reader comments
0 contributions