Skip to main content

MWITIKIO HAFIFU WA TOHARA WAZUA JAMBO MPIMBWE, MADIWANI WAITAKA SERIKALI IPUNGUZE GHARAMA

Na Daniel Gahu - Katavi.

MWITIKIO HAFIFU WA TOHARA WAZUA JAMBO MPIMBWE, MADIWANI  WAITAKA SERIKALI IPUNGUZE GHARAMA

Na Daniel Gahu - Katavi.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi limeeleza wasiwasi wake kuhusu mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupata huduma ya tohara katika vituo vya afya vya umma, huku likidai kuwa gharama za huduma hiyo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wengi.

Madiwani hao wamejadili suala hilo katika kikao cha baraza, wakieleza kuwa takwimu zilizowasilishwa zinaonyesha idadi ya wanaume na watoto wanaofika kupata huduma ya tohara imeendelea kupungua tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa madiwani, wamesema moja ya sababu kubwa inayochangia hali hiyo ni gharama za huduma hiyo, ambazo kwa sasa ni shilingi elfu 30 kwa mtu mzima na shilingi elfu 15 kwa mtoto katika hospitali za Serikali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.

Kutokana na hali hiyo, madiwani wameiomba Serikali kuingilia kati na kutafuta suluhisho litakalowezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma hiyo muhimu ya afya kwa gharama nafuu, hatua ambayo wanaamini itaongeza mwitikio wa wananchi na kuchangia katika kuimarisha afya ya jamii.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wamefafanua kuwa kupungua kwa mwitikio wa wananchi si kwa sababu ya ubora wa huduma, bali kunahusishwa na mabadiliko ya mfumo wa ufadhili wa huduma hiyo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri amesema kuwa hapo awali huduma ya tohara ilikuwa ikitolewa bila malipo kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani pamoja na mashirika yaliyokuwa yakitekeleza programu mbalimbali za afya nchini. Lakini baada ya ufadhili huo kusitishwa, huduma hiyo ilianza kutolewa kwa mfumo wa kuchangia gharama, jambo ambalo limeathiri idadi ya wanaojitokeza.

"Ikumbukwe huduma ya tohara ilikuwa ikitolewa bure kipindi cha nyuma, lakini mara baada ya ufadhili wa Serikali ya Marekani kusitishwa na huduma hiyo kuanza kutolewa kwa gharama, wanaume wengi wameacha kujitokeza kwa wingi kama ilivyokuwa awali."

Kwa mujibu wa wataalamu hao, kusitishwa kwa ruzuku kutoka kwa Serikali ya Marekani kulisababisha pia mashirika mbalimbali yaliyokuwa yakitoa huduma za tohara bila malipo nchini kusitisha shughuli hizo, na kuiacha Serikali kubeba jukumu hilo kupitia vituo vyake vya afya.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, ambaye pia ni Diwani, Mheshimiwa Silas Ilumba, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na timu ya wataalamu kupitia upya viwango vya gharama za huduma hiyo ili kuona uwezekano wa kuvipunguza na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma hiyo.

Katika mapendekezo yaliyowasilishwa na Baraza la Madiwani, imependekezwa gharama ya tohara kwa mtu mzima ishushwe kutoka shilingi elfu 30 hadi shilingi elfu 20, huku gharama kwa watoto ikipunguzwa kutoka shilingi elfu 15 hadi shilingi elfu 10.

Madiwani wanaamini kuwa hatua hiyo itaongeza mwitikio wa wananchi, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kusaidia juhudi za Serikali katika kuzuia maambukizi ya magonjwa pamoja na kuimarisha afya ya uzazi kwa wanaume.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.