Na Cecilia Shiratu, Bhiharamulo - Kagera.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, zimehitimishwa Wilayani Biharamulo mkoani Kagera, baada ya kuzindua, kukagua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2, ikiwemo sekta za maji, elimu, afya na uchumi.
Ukiwa Wilayani humo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang'onda, alizindua vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyakahula, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali na wananchi kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, Mwenge huo umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Zahanati ya Maragala, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mwang'onda, pia amegawa vyandarua kwa akina mama wajawazito, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuhamasisha matumizi ya vyandarua na kuimarisha afya ya mama na mtoto, pamoja na kugawa majiko ya gesi kwa mama lishe na baba lishe katika kata ya biharamulo mjini ikiwa ni ishara ya kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kuhakikisha viti na meza vinawekwa ndani ya siku saba katika vyumba viwili vya madarasa vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kagango ili vianze kutumika.
Vyumba hivyo, vimekamilika kutokana na ushirikiano wa nguvu za wananchi na Serikali, hivyo agizo hilo linalenga kuhakikisha wanafunzi wanaanza kutumia madarasa hayo katika mazingira bora ya kujifunzia.

Mbio hizo zimeendelea kuwa sehemu ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo, kuimarisha uwajibikaji na kuhimiza matumizi bora ya rasilimali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kudumisha amani na mshikamano.

Discussion
Reader comments
0 contributions