Skip to main content

MWENGE WA UHURU WAHITIMISHA MBIO ZAKE TABORA; MIRADI 55 YA TSH. BILIONI 35.6 YAANGAZIWA.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Beno Malisa, amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Mwanamvua Mrindoko katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Michezo wa Shule ya Msingi Kamsisi, Wilaya ya Mlele Mkoani humo.

MWENGE WA UHURU WAHITIMISHA MBIO ZAKE TABORA; MIRADI 55 YA TSH. BILIONI 35.6 YAANGAZIWA.
Studio Narration JAMBO FM

MWENGE WA UHURU WAHITIMISHA MBIO ZAKE TABORA; MIRADI 55 YA T...

0:00 --:--

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Beno Malisa, amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Mwanamvua Mrindoko katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Michezo wa Shule ya Msingi Kamsisi, Wilaya ya Mlele Mkoani humo.

Makabidhiano hayo yamehitimisha safari ya Mwenge wa Uhuru Mkoani Tabora, baada ya kukimbizwa kwa siku nane na kufikia Wilaya zote za Mkoa huo, ukiangazia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa makabidhiano hayo, Mwenge huo umefikia na kuangazia miradi 55 yenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 35.6, huku ukikimbizwa kwa umbali wa jumla ya kilomita 1,616.2.

Safari hiyo ilianzia Wilaya ya Kaliua na kuendelea katika Wilaya za Urambo, Uyui, Nzega, Igunga, Tabora na Sikonge, kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Katavi.

Katika kipindi hicho, Mwenge wa Uhuru uliweka mawe ya msingi, kuzindua, kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, maji, barabara, mazingira, uwekezaji, nishati safi na uwezeshaji wa vijana kiuchumi.

Mbali na kukagua maendeleo ya miradi, ziara hiyo ilitoa nafasi ya kutathmini ubora wa kazi zinazofanyika pamoja na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali, Halmashauri, wananchi, wahisani na sekta binafsi.

Wasimamizi wa miradi wamesisitizwa kuhakikisha kazi zinakamilishwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili miundombinu hiyo iweze kutoa huduma zilizokusudiwa na kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.

Akizungumza katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa na Mwenge huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda amesisitiza wananchi kuwa na jukumu la kulinda na kutunza miundombinu ya umma inayojengwa kwa fedha za Serikali na wadau mbalimbali.

Mwang’onda pia amehimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu, huku akiwataka kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha yao.

Katika safari yake Mkoani Tabora, Mwenge wa Uhuru umeendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiafya, yakiwemo mapambano dhidi ya Rushwa, Ukimwi, Malaria, Matumizi ya Dawa za Kulevya na Utapiamlo.

Aidha, wananchi wameendelea kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na salama katika kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa afya na mazingira.

Baada ya kukabidhiwa, Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake Mkoani Katavi, ukiwa na lengo la kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mshikamano wa kitaifa na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 zinaongozwa na kaulimbiu: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.