Viongozi na wadau mbalimbali Jijini Mwanza wamekubaliana kuendelea kushirikiana na MWAUWASA ili kuboresha huduma ya maji kwa wakazi. Wito huo umetolewa katika mkutano maalum uliowakutanisha MWAUWASA na wadau kutoka makundi mbalimbali kujadili hali ya sasa ya huduma ya maji, pamoja na mipango iliyopo na inayoendelea kutekelezwa
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Amiri Mkalipa tarehe 7 mwezi huu amesisitiza kuwa sambamba na mipango mizuri na jitihada za MWAUWASA, ushiriki wa wadau ni muhimu ili mipango hiyo itimie na iwe na matokeo halisi. Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya maji kupitia MWAUWASA, lakini wadau wanapaswa kuunga mkono kwa kulinda miundombinu na kulipia bili za maji kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Mashaka Sitta, akiwasilisha taarifa kwa wadau ameeleza kuwa MWAUWASA ina mipango ya muda mfupi, wa kati na ya kudumu inayolenga kuboresha huduma ya maji Jijini Mwanza. Mipango hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu ya maji.
Mkutano huo umehusisha viongozi wa serikali, vyama vya siasa, viongozi wa kidini na mila, wafanyabiashara, menejimenti ya MWAUWASA, wanahabari, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi watumiaji wa huduma ya maji. Wadau wote wameazimia kutoa ushirikiano kamili kwa MWAUWASA ili kulinda rasilimali ya maji na kuhakikisha mipango ya kuboresha huduma inafanikiwa.



Discussion
Reader comments
0 contributions