Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CP Salum Hamduni amewahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kupata huduma za matibabu kwa wakati na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia.
Hamduni ameyasema hayo Oktoba 22, 2026 wakati akizindua awamu ya pili ya usajili wa bima hiyo mkoani Mwanza, yenye kaulimbiu isemayo "Bimika na Fahari Afya."

Amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kubaguliwa kwa misingi ya kipato.
Ameeleza kuwa afya ni mtaji wa maendeleo, kwani mwananchi mwenye afya njema anaweza kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuinua maisha yake.
Aidha, CP Hamduni amezitaka halmashauri kuweka mikakati madhubuti ya usajili na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima hiyo.
Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha kila mwananchi anayestahili anafikiwa na mpango huo bila kuachwa nyuma.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mwanza Bw. Isaack Katemba amesema katika awamu ya kwanza mkoa ulilenga kusajili kaya 19,345 ambapo kaya 14,589 zimesajiliwa sawa na asilimia 75.4.
Katika awamu ya pili mkoa unalenga kusajili kaya 35,642 ambapo kaya 1,790 tayari zimesajiliwa sawa na asilimia 5, huku wanufaika 2,870 kati ya 90,981 waliolengwa wamesajiliwa sawa na asilimia 3.2.
Ameongeza kuwa wananchi wanaweza kujiunga kupitia kifurushi cha Fahari Afya kwa Shilingi 150,000 kwa mwaka kwa kaya yenye watu wasiozidi sita, na vikundi vyenye watu wasiopungua 10 vinaweza kujiunga na Umoja Afya kwa Shilingi 60,000 kwa mwaka.
Akitoa ushuhuda, Mnufaika wa Bima ya Afya kwa Wote Saimoni Makolele mkazi wa Mtaa wa Kabambi Kiseke, Ilemela, amesema bima hiyo imemsaidia yeye na watoto wake kupata huduma za matibabu bila gharama za moja kwa moja wanapohitaji matibabu.
Discussion
Reader comments
0 contributions