Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza utakuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yatakayofanyika kuanzia Mei 18 hadi 21, 2026 katika Viwanja vya Nane Nane Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela.
Akizungumza Mei 17, 2026 na Waandishi wa Habari ofisini kwake, RC Mtanda amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha uhifadhi wa Ziwa Victoria pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali zake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema Siku ya Ziwa Victoria imeanzishwa kufuatia azimio la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ambapo Mei 21 ya kila mwaka itakuwa siku maalum ya kutambua mchango wa ziwa hilo kwa nchi wanachama.
Kadhalika ameeleza ziwa Victoria lina ukubwa wa kilomita za mraba 68,800 ambapo Tanzania inamiliki asilimia 51, Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia 6. Zaidi ya wananchi milioni 45 wanategemea ziwa hilo kupitia shughuli za uvuvi, usafirishaji, utalii, kilimo na uzalishaji wa umeme.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni: "Maji Yetu, Mustakabali Wetu: Tuungane kwa Uendelevu wa Bonde la Ziwa Victoria," ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kulinda mazingira na kukuza uchumi wa buluu.
Discussion
Reader comments
0 contributions