Na Saulo Stephen - Singida.
Watanzania wametakiwa kuendelea kulinda amani na utulivu nchini ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayoboresha maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang'onda, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kinyagigi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Mwang'onda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, akieleza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo yanayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.

"Ili haya mambo mazuri tunayoyaona katika maeneo yetu yaendelee kuja, Mheshimiwa Rais anawaomba sana Watanzania kulinda amani na utulivu. Nchi ikiwa tulivu, itaendelea kuleta maendeleo makubwa zaidi ya haya ambayo tayari tumeyaona," amesema Mwang'onda.
Aidha, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa mradi huo, hususan kukamilika kwa jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), ambalo litarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kinyagigi na maeneo jirani.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya kwa wananchi, huku akieleza kuwa Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwa kuridhishwa na ubora na maendeleo ya mradi huo.
Baada ya hotuba hiyo, Mwang'onda aliweka rasmi jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kinyagigi, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Discussion
Reader comments
0 contributions