Na Saulo Stephen - Singida.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari amesema Magari manne yaliyorejeshwa na kukabidhiwa kwa Kampuni ya SEMA LIMITED, ni matokeo ya Kliniki ya Kisheria bila malipo iliyofanyika kuanzia Aprili 19 - 25, 2025 Mkoa wa Singida.
Akizungumza katika Hafla hiyo Johari amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipokea lalamiko la Meneja wa Karakana wa Sustainable Environment Management Action (SEMA), Lameck Muyanzi aliyelalamikia Kampuni ya TAOMTRA Limited (Hussein Mjili na Getruda Agripa Mwashambwa - Dalali wa Mahakama) kwa kukamata magari matano ya Kampuni ya SEMA na kuyauza magari husika isivyo halali.

"Tulipokea lalamiko kutoka Kampuni ya SEMA na nilikabidhi kwa watalaamu kwa ajili ya kulishughulikia na matokeo yake ndio haya mnayaona leo hapa "Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha ameongeza kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Singida pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Singida, ilifanya jitihada za kuyarejesha magari hayo kwa kampuni ya SEMA, huku akisisitiza ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali itaendelea na utaratibu wa kutembelea maeneo mbalimbali nchini na kutatua kero za kisheria zinazowakabili wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Singida ,Godwin Gongwe amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi hususani wa Mkoa wa Singida.
Awali akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Neema Ringo amezishukuru Taasisi mbalimbali zilizoshiriki katika kushughulikia lalamiko hilo na kuweza kulitatua na kuwezesha Kampuni ya SEMA kurejeshewa magari yaliyokuwa yameshikiliwa na Kampuni ya TAOMTRA Limited.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya SEMA, Ivo Manyaku amemshuruku Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushugulikia changamoto iliyokuwa inawakabili na kufanikisha kurejeshewa magari ya Kampuni ya SEMA yaliyokuwa yanashikiliwa na Kampuni ya TAOMTRA Limited.
Kampuni ya SEMA Limited imefanikiwa kurejeshewa jumla ya magari manne (4) ambayo ni Toyota Land Cruiser S/Wagon lenye namba za usajili T465 AED; Isuzu Winch lenye namba za usajili T418 AED; Isuzu Tipa lenye namba za usajili T423 AED na Land Rover 101 Station Wagon lenye namba za usajili T412 AED.

Discussion
Reader comments
0 contributions