Na Adam Msafiri, Rorya – Mara.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja zinatatuliwa changamoto zote zinazosababisha upungufu wa maji katika mji wa Shirati, Wilaya ya Rorya, ili wananchi waondokane na mgao wa maji ambao umekuwa kero ya muda mrefu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Obwere, Shirati, Dkt. Nchemba amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miradi ya maji kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo haikubaliki kuona wananchi wakiendelea kukosa huduma hiyo kutokana na uzembe wa watendaji.

Amesisitiza kuwa viongozi na watendaji wa sekta ya maji wanapaswa kuhakikisha miundombinu iliyojengwa inatoa huduma inayokusudiwa, badala ya kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Katika mkutano huo, wananchi wa Shirati wamebua changamoto mbalimbali zinazoendelea kuwakabili, ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, wakiiomba Serikali kuingilia kati na kutoa suluhisho la kudumu.

Mbali na suala la maji, Waziri Mkuu pia ametoa maagizo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara kuhakikisha mchakato wa kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Utegi–Shirati unafanyika kwa haraka ili kuanza utekelezaji wa mradi huo, ambao wananchi wamekuwa wakiusubiri kwa muda mrefu.
Dkt. Nchemba anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, amekuwa akikutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kutoa maelekezo ya kuzitatua.
Discussion
Reader comments
0 contributions