Baadhi ya vijana wilayani Musoma mkoani Mara, wameiomba Serikali kuongeza juhudi za utoaji elimu kuhusu upatikanaji wa mikopo ya vijana inayotolewa kupitia Wizara ya Vijana, ili kuhakikisha kundi kubwa zaidi linafikiwa na kunufaika na fursa hiyo.
Ombi hilo linakuja wakati Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mfuko wa zaidi ya shilingi bilioni 200, unaolenga kuchochea uanzishaji na uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Baadhi ya vijana akiwemo Frank Mafuru na Samwel Ngagani wakizungumza na Tovuti hii,wamesema mikopo hiyo ni fursa muhimu itakayowawezesha kujiajiri,kuongeza kipato chao binafsi pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa,lakini bado uelewa kuhusu namna ya kuipata haujafikia wengi.
Hata hivyo, vijana wengine wameeleza kutofahamu kabisa uwepo wa fursa hiyo,wakisisitiza haja ya Serikali kushusha elimu hadi ngazi ya jamii ili kuwafikia vijana wengi zaidi, hususan walioko vijijini.

Kutokana na hali hiyo, Serikali Musoma imeanza kuchukua hatua ambapo Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amewahakikishia vijana kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya utoaji taarifa na urahisishaji wa upatikanaji wa mikopo hiyo,ili iweze kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana,kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya Taifa.
Discussion
Reader comments
0 contributions