Na Clavery Christian, Muleba - Kagera.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Isaya Mbenje, ametoa wito kwa maafisa uvuvi kuhakikisha wanazitunza na kuzitumia kikamilifu boti mbili mpya za kisasa aina ya fiber boat zilizopokelewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uvuvi pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza wakati wa kupokea boti hizo zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89, Mbenje amesema matumizi sahihi ya vifaa hivyo yataziwezesha kudumu kwa muda mrefu huku vikichangia kuongeza ufanisi katika kulinda rasilimali za maji na kuwasaidia wavuvi wanaofuata sheria kufanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye tija.

Aidha, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za halmashauri kuongeza uwezo wa kusimamia na kufuatilia shughuli za uvuvi pamoja na kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za uvuvi zinafuatwa ipasavyo katika maeneo yote ya ziwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, ndugu Evart Kagaruki, amesema ununuzi wa boti hizo utaongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanyika ziwani ikiwemo doria za uvuvi pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Kagaruki ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kuridhia ombi la ununuzi wa boti hizo na kupitisha fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Ameongeza kuwa baada ya kupokelewa kwa boti hizo, idadi ya boti zinazomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imefikia saba.

Naye Afisa Uvuvi wa Wilaya hiyo, ndugu Wilfred Timbendana, amesema boti hizo zitasaidia kufika katika maeneo korofi ambayo awali yalikuwa hayafikiki kwa urahisi, hususan katika visiwa vya Goziba na maeneo mengine ya ziwani, hali itakayorahisisha utekelezaji wa doria na usimamizi wa shughuli za uvuvi.
Discussion
Reader comments
0 contributions