Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amesisitiza kuwa maelekezo yanayotolewa katika vikao yanapaswa kuchukuliwa kwa mtazamo chanya na watumishi, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
DC Wella ameyasema hayo katika Kikao cha Tathmini ya Lishe cha Wilaya kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Tabora.

Amesema kuwa maelekezo yanayotolewa katika vikao hayana lengo la kupelekeshana au kulaumiana, bali ni kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa.
“Tunapopeana maelekezo, ndugu zangu watumishi, hatuna lengo la kupelekeshana. Lengo ni moja tu—kuwahudumia wananchi wetu. Hivyo, maelekezo yote tunayotoa tuyachukulie kwa mtazamo chanya ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea.”

Katika kikao hicho, DC Wella pia amewapongeza watendaji kwa namna wanavyoendelea kusimamia masuala ya lishe katika kata zao, hususan utekelezaji wa mpango wa chakula shuleni.
Aidha, amewasisitiza watendaji wa kata ambazo bado mwitikio wa wananchi katika suala la chakula shuleni si mkubwa kuandaa mikutano ya wananchi na kumualika ili aweze kuzungumza nao na kuhamasisha ushiriki wao katika kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni.

Discussion
Reader comments
0 contributions