Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Wito umetolewa kwa wakulima wa zao la pamba kutunza zao hilo katika mazingira ya usafi, ili pamba itakayotoka Tanzania na kwenda kuuzwa nje iwe na ubora wa kimataifa kwani pamba yote nchini kwa asilimia 70 inauzwa nje ya nchi ,hivyo huingia katika ushindani na pamba inayozalishwa kutoka katika nchi zingine.
Rai hiyo imetolewa na kaimu mkurugenzi wa bodi ya pamba kanda ya magharibi Renatus Filbert wakati akizungumza na jambo media ofisini kwake kuhusiana na kuanza kwa msimu wa ununuzi wa pamba kwa mwaka 2026 na kuanisha kuwa zao la pamba ni zao la kibiashara hivyo wakulima waichambue pamba hiyo na kutokuivuna na vikonyo.

Katika hatua nyingine Fibert ametoa onyo kwa wanunuzi wa pamba zikiwemo AMCOS kuhakikisha mizani zipo sahihi pasipokuwaibia wakulima lakini pia kuwalipa wakulima fedha mara wanapoleta pamba yao pasipo kuwakopa kwani mnunuzi yeyote atakayebainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake huku akianisha kuwa bei elekezi kwa zao la pamba katika msimu huu ni shilingi 1240.
“Nizitahadharishe kabisa AMCOS msimu uliopita kuliwa na udanganyifu mwingi kwa wakulima hasa kwa upande wa mizani wasijaribu kufanya hivyo kwani serikali imejipanga na pindi watakapobainika watafikishwa katika mkono wa sharia na watakuwa ni wahujumu uchumi kama wahujumu wengine,“ amesema Filbert .

Kufuatia onyo hilo jambo media ikafunga safari mpaka kwa wanunuzi na wachakati wa zao la pamba kutoka kampuni ya mashati investment wanaofanya shughuli zao katika wilaya ya Shinyanga na kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa kampuni hiyo Novatus Shirima ili kufahamu wanazungumziaje onyo hilo lililotolewa na bodi ya pamba, ambapo amesema kuwa wamehakiki mizani hivyo watapima kwa ufasaha na hakuna mkulima atakayekopwa pamba yake.
"Kampuni ya Mashati tuko vizuri na tumejiandaa vyema na soko, tunawakaribisha wakulima wafike kwenye vituo vyetu kuuza pamba, na tunawahakikishia kuwa tunaponunua pamba kwa mkulima, tunampatia pesa yake papo hapo bila kuchelewa," amesema Shirima.

Nao baadhi ya wakulima wa pamba katika kijiji cha Mwalukwa akiwemo Masanja Dashina,Ringobet Lugembe na Sato Richard ambao jambo media imekuta wameleta pamba yao katika AMCOS ya mashat investment kuuza, wamekiri kuridhishwa na bei elekezi iliyotolewa na serikali pamoja na huduma waliyopata katika AMCOS hiyo.
Lakini pia wakulima hao wamekiri kwamba tayari wamelipwa fedha zao huku wakiwataka wakulima wengine kuleta pamba ili wapate fedha za kununua mahitaji kabla ya mfumuko wa bei.



Discussion
Reader comments
0 contributions