Na Daniel Gahu - Katavi.
Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, imewataka wananchi wa Mkoani hapa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano kwa kuepuka vichochezi vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa Mkoa wa Katavi pamoja na nchi kwa ujumla.
Ametoa rai hiyo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ambapo amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, na kuepuka kushiriki maandamano au vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na amani.

"Vitendo vya uchochezi vinavyolenga kuvuruga utulivu wa nchi ni kinyume na sheria pamoja na maelekezo ya viongozi wakuu wa Serikali, Serikali itaendelea kuhakikisha sheria zinafuatwa ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao," amesema Mhe. Mrindoko
Amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi unaendelea kuwa salama, huku akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo wakati wote katika maeneo yote ya mkoa.
Aidha, ametoa onyo kwa mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani au kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika bila upendeleo.
Akihitimisha, Rc Mrindoko amewahimiza wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku za kiuchumi kwa amani na utulivu, ili wajipatie kipato, kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Katavi na Taifa kwa ujumla.
Discussion
Reader comments
0 contributions