Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema eneo la uchimbaji la Mgodi wa Msasa Gold Mine uliopo wilayani Bukombe mkoani Geita litaendelea kuwa mali ya wachimbaji wadogo, akisisitiza kuwa hakuna mpango wowote wa kuwaleta wachimbaji wakubwa katika eneo hilo.
Ametoa maelezo hayo alipofanya ziara ya kujionea hali ya usalama katika mgodi huo akiwa ameambatana na kamati ya usalama ya mkoa huo na kufafanua kwamba hakuna mpango wowote wa kupelekea wachimbaji wakubwa katika mgodi huo wenye zaidi ya maduara 1300.

“Hakuna mpango wowote,wala mpango wa kutengeneza,sijui kuleta wachimbaji wakubwa,sijui kuwaondoa wachimbaji wadogo,Msasa itaendelea kuwa ya wachimbaji wadogo ili waweze kuendelea kujiletea fedha”
Aidha RC Shigela amesisitiza kuwa agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa kama mgodi huo hauna madhara yatokanayo na uchimbaji katika mgodi huo,mgodi husika usifungwe limetekelezwa.

Wakati huo huo amewapongeza wananchi mkoani Geita ikiwa ni pamoja na wachimbaji wadogo kwa kudumisha amani na utulivu katika sikukuu ya sabasaba kwa kupuuza vitisho na kuwapuuza wanaohamasisha vurugu nchini.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,(SACP) Safia Jongo amesema Jeshi la Polisi litaendelea kulinda usalama wa raia na mali zao akiwataka kuendela kufanya kazi na kuahidi kwamba jeshi hilo litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama.

“Ninachoweza kusema ni kwamba endeleeni kupiga kazi,kutafuta hela,ulinzi na uslama niachieni mimi na ninawahakikishia kwamba hali ya ulinzi na usalama hapa itaendelea kuwa ilivyo”
Kwa upande wao wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Geita wameipongeza Serikali kwa kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba, huku wakiahidi kuendelea kushiriki katika kulinda amani na utulivu wa nchi.

Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Geita ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Martine Shigela imetembelea maeneo mbalimbali ya shughuli za wananchi ili kujionea hali ya usalama ambapo kupitia ziara hiyo,kamati ilishuhudia wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida.

Discussion
Reader comments
0 contributions