Na Gideon Gregory - Dodoma.
Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Barrick kupitia ubia wake na Twiga Minerals, imezindua awamu ya pili ya mradi wa Barrick–Twiga Future Forward Education Program katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa, mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kupitia ujenzi wa madarasa, mabweni na majengo ya vyoo katika shule mbalimbali za sekondari nchini, hususani zinazohudumia wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu inayowezesha wanafunzi na walimu kupata mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

"Kufuatia makubaliano haya yaliyofikiwa kati ya Barrick na Serikali mwaka 2023, kampuni yetu ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule mbalimbali za sekondari nchini.
Amesema katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa, mradi huo unahusisha ujenzi wa madarasa Sita na mabweni mawili yaliyokamilika, yakiwa na madawati na vitanda kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita.
Pia, dkt. Ngido amesema mradi huo unatarajiwa kujenga madarasa 1,090, mabweni 270 pamoja na majengo ya maliwato na vyoo 1,640 katika shule 161 nchini, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi takribani 190,000.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe, ameipongeza Barrick kwa uwekezaji huo na kusema sekta ya elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo ili iweze kuwanufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo.
Prof. Shamdoe amesema Elimu si matumizi bali ni uwekezaji wa kimkakati kwa rasilimali watu pia aliishukuru BARRICK kwaushirikiano mzuri WA kuleta maendeleo katika jamii
Naye Meneja wa Fedha wa Barrick, Penina Kituku, amesema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika elimu kwa kuwa ndiyo njia ya kufungua fursa kwa vijana wa Kitanzania na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia kizazi chenye maarifa na ujuzi.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo, wakisema mabweni na madarasa mapya yanaboresha mazingira ya kujifunzia, kuongeza hali ya kusoma na kuwapa motisha ya kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
Kupitia awamu ya pili ya Barrick–Twiga Future Forward Education Program, Serikali na Barrick zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, huku zikiweka msingi wa kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa maelfu ya wanafunzi nchini.
Discussion
Reader comments
0 contributions