Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Rajab Magaro, Juni 25, 2026 ametembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa Nkome lililopo Kata ya Nkome, Wilaya ya Geita, kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo muhimu unaotarajiwa kuchochea ukuaji wa shughuli za biashara na maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Magaro amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya RIN Contractor and General Supplies Company Ltd, kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika na kukabidhiwa kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai 2026.

Amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na miundombinu yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi mbele ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi wa mradi Eng. Edson Missana, amesema soko hilo la kisasa litakuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara na watumiaji zaidi ya 80 kwa wakati mmoja.

Aidha, amesema soko hilo limezingatia viwango vya kisasa vya miundombinu, likiwa na jengo la vyoo lenye matundu 10 pamoja na mabafu maalumu kwa ajili ya matumizi ya wafanyabiashara na wananchi watakaokuwa wakilitumia.
Kukamilika kwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha maendeleo endelevu katika Wilaya ya Geita.

Mradi wa Soko la Kisasa Nkome unafadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa gharama ya Shilingi 473,909,792.82 hadi kukamilika kwake ukitarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha biashara, kuongeza fursa za ajira na kuinua kipato cha wananchi wa Kata ya Nkome na maeneo jirani.

Discussion
Reader comments
0 contributions