Katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani leo Agosti 12, 2026, Taasisi isiyo ya kiserikali ya Fadhili Teens Tanzania, imezindua mradi maalumu wa kutoa motisha kwa Walimu wa Shule za Sekondari katika Halmashauri za Magu na Buchosa mkoani Mwanza.
Uzinduzi wa mradi huo, umefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu na kuzinduliwa rasmi na Mkurugenzi Mohamed Ramadhan. ukilenga kuongeza hamasa ya ufundishaji na kuboresha ufaulu wa Wanafunzi zaidi ya 10,000.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ramadhan amewataka wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu na wazazi ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.
Amesisitiza kuwa, mafanikio ya Mwanafunzi yanategemea kwa asilimia 75 ya juhudi binafsi, huku asilimia 25 zikichangiwa na mazingira yanayomzunguka, ikiwemo uwepo wa walimu wenye motisha, miundombinu bora na mazingira mazuri ya kujifunzia.

Akieleza malengo ya mradi huo, Salome Ndimila kutoka Fadhili Teens Tanzania amesema utatekelezwa katika shule 20, ambapo shule 10 zinatoka Halmashauri ya Buchosa na shule 10 nyingine kutoka Halmashauri ya Magu.
Ameongeza kuwa, mradi huo unatarajiwa kuwafikia walimu 300, wanafunzi 10,000 pamoja na wazazi 8,000 ambapo taasisi hiyo itatoa mafunzo ya kujengea uwezo Walimu na jamii kwa kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuboresha mbinu za ufundishaji.

Baadhi ya washiriki wa mradi huo, akiwemo Mwl. Kaombwe Edward na Mwl. Christina Nisa wameishukuru Fadhili Teens Tanzania kwa kuanzisha mradi huo na kuahidi kutoa ushirikiano.
Uzinduzi huo, unakuja wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Vijana Duniani, ikisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika vijana kupitia elimu bora na walimu wenye motisha ili kujenga kizazi cha kesho chenye ujuzi na maadili.
Discussion
Reader comments
0 contributions