Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Katibu tawala mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni leo ,amezindua rasmi mradi wa malezi na makuzi ya mtoto unaotekelezwa na kanisa la Anglikana Tanzania dayosisi ya Shinyanga wenye lengo la kuboresha maendeleo ya awali ya ukuaji wa mtoto kupitia malezi bora,ushiriki wa jamii na kuimarisha ustawi wa uchumi wa kaya.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo CP Hamdun amesema ustawi wa mtoto katika umri kuanzia o mpaka miaka 3 ni jambo la msingi Katika kujenga taifa lenye rasilimali watu bora na kuwataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika mazingira bora na salama ya kujifunza.
“Kupitia mradi huu tunatarajia kuona ongezeko la uelewa wa wazazi na walezi kuhusu malezi bora kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa afya na lishe ya watoto kuimarika katika mkoa wa Shinyanga,“ amesema CP Hamduni.

Amesema mradi huo unakwenda sambamba na jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za awali za maendeleo ya mtoto kwa kuhakikisha watoto wanapata huduma za afya na lishe bora kwa kuzingatia ustawi wa afya ya mwili na akili pia.
Kwa upande wake askofu wa kanisa la anglikana Tanzania dayosisi ya Shinyanga Johnson Chinyong’ole mradi huo utatekelezwa katikahalimashuri ya wilaya ya Kishapu katika vijiji vya Mayanji,Bulimba,Mwaweja na Negezi na kwamba utekelezaji wa mradi huo ni agizo la Mungu kwani Yesu alisema amekuja duniani ili watu wawe na uzima tele hivyo uzima ni pamoja na ustawi wa afya njema.
Askofu Chinyong’ole amesema mradi huo unaenda kutekelezwa kwa kushirikiana na jamii pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya afya ili kuendelea kuongeza uelewa kuhusu malezi mazuri ya watoto pamoja na haki zao ili kuboresha mazingira ya ukuaji.

Naye mganga mkuu mkoa wa Shinyanga Dr Honaratha Rutatinisibwa amesema kupitia mradi huo jamii inakwenda kujengewa uelewa mkubwa kuhusiana na malezi ya mtoto na kwamba utakwenda kupunguza tatizo la udumavu pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto.
Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, afya na makuzi ya mtoto na unatajwa kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa malezi bora na yenye usatwi kwa mtoto katika jamii.
Discussion
Reader comments
0 contributions