Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Afya na kufanya nao mazungumzo ofisini kwake, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa Mradi wa Beginning unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, ukilenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto mchanga mkoani Tabora.
Mradi huo unatarajiwa kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo 30 vya kutolea huduma za afya vitakavyobainishwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Tabora, kwa kuweka mazingira bora na salama ya utoaji wa huduma hizo.
Akizungumza na wataalamu kutoka Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Halmashauri (Council Health Management Teams – CHMTs) za Mkoa wa Tabora, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala, amesema mradi huo utajikita katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, ikiwemo upatikanaji wa majengo na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya huduma za mama na mtoto mchanga.
Aidha, Dkt. Bundala ameeleza kuwa mradi huo utaimarisha uwezo wa watoa huduma kupitia mafunzo ya kitaalamu, kuongeza nguvu kazi ya wataalamu wa afya kwa utaratibu wa ajira za mikataba, pamoja na kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika vituo vitakavyonufaika na mradi huo.
Utekelezaji wa Mradi wa Beginning unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora, hususan wanawake wajawazito, akina mama na watoto wachanga, kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora, salama na kwa wakati, hatua inayolenga kupunguza changamoto na hatari zinazohusiana na ujauzito, kujifungua na afya ya watoto wachanga.
Discussion
Reader comments
0 contributions