Skip to main content

MPIMBWE YAFUNGUA MILANGO BIASHARA YA CABON

Na Daniel Gahu - Katavi.

MPIMBWE YAFUNGUA MILANGO BIASHARA YA CABON

Na Daniel Gahu - Katavi.

Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe iliyopo mkoani Katavi imechukua hatua muhimu kuelekea biashara ya kaboni baada ya kuingia makubaliano ya awali na kampuni ya Prime Carbon Tanzania kwa ajili ya kuanzisha utekelezaji wa mradi huo katika vijiji 15 na eneo la Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori (WMA) Mpimbwe.

Makubaliano hayo yamefanyika katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe, yanatarajiwa kufungua fursa mpya za mapato kwa wananchi kupitia uhifadhi wa misitu, sambamba na kuimarisha utunzaji wa mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Walioshiriki katika hafla ya makubaliano hayo ni viongozi wa Prime Carbon Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamim Mwariko, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Kasansa, Silas Ilumba.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Prime Carbon Tanzania itaanza utekelezaji wa hatua za awali za mradi ikiwemo kutoa mafunzo kwa Vikundi vya Walinzi wa Misitu Vijijini (VGS), kufanya tathmini ya kiwango cha kaboni kilichopo katika misitu, kuandaa mpango wa usimamizi wa misitu na kufanya mikutano ya ushirikishwaji wa wananchi, makundi maalumu na wadau wa mazingira katika vijiji vinavyonufaika.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza mapato yatakayotumika kugharamia miradi ya maendeleo katika vijiji na Halmashauri ya Mpimbwe, huku ukiimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Pia unatarajiwa kuongeza idadi ya wanyamapori na kuimarisha shughuli za utalii, pamoja na kuchangia kuboresha hali ya hewa itakayosaidia uzalishaji wa kilimo kupitia upatikanaji wa mvua.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Silas Ilumba, ameipongeza Prime Carbon Tanzania kwa kuichagua Mpimbwe kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuharakisha hatua za utekelezaji.

"Tunatarajia mradi huu uanze kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na mapato yatokanayo na biashara ya kaboni. Haya ni maendeleo yatakayoongeza ari ya wananchi kushiriki katika uhifadhi wa mazingira," alisema Ilumba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Shamim Mwariko, amesema halmashauri hiyo inaendelea kufungua milango kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali kutokana na fursa zilizopo.

Ametaja uwekezaji katika kiwanda cha kuzalisha vifungashio vya mazao kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa, akieleza kuwa Mpimbwe ni mzalishaji mkubwa wa mpunga na mahindi, lakini bado wakulima na wafanyabiashara hutegemea vifungashio vinavyotoka nje ya mkoa.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, pamoja na kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa halmashauri.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.