Na Daniel Gahu - Katavi.
Katika kuhakikisha Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe Manispaa ya Mapanda zinaimarika Idara ya afya imeendesha mafunzo maalum ya uingizaji wa taarifa za lishe katika mifumo ya DHIS2 na IMES kwa Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji. Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi wa taarifa za lishe na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga na kutekeleza hatua mbalimbali za maendeleo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda yakihusisha watendaji kutoka maeneo mbalimbali huku Lengo kuu likiwa ni kuwajengea uwezo washiriki katika ukusanyaji, uingizaji na usimamizi wa taarifa za lishe kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Gwalusajo Kapande, amewasisitiza watendaji hao kuyapa uzito mafunzo hayo kwa kuwa wao ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika ngazi za jamii.
Amesema uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mifumo ya DHIS2 na IMES utawasaidia watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuwawezesha kuwajengea uwezo watendaji wengine katika maeneo yao kwa haraka na kwa usahihi.

Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Manispaa ya Mpanda, Mwanaid Said, amesema kuwa matumizi sahihi ya mifumo hiyo yataongeza ubora wa taarifa zinazokusanywa na kuchambuliwa, jambo litakalosaidia katika kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha huduma za lishe na afya kwa wananchi.
Ameongeza kuwa mifumo ya DHIS2 na IMES ina umuhimu mkubwa katika kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na za wakati kuhusu hali ya lishe katika jamii, kufuatilia utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe, pamoja na kusaidia viongozi na wataalamu kupanga mikakati yenye tija kwa maendeleo ya sekta ya afya na ustawi wa wananchi.



Discussion
Reader comments
0 contributions