Wananchi wa Manispaa ya Mpanda wamepongeza hatua ya Halmashauri kuanzisha mashindano ya usafi wa mazingira katika ngazi za mitaa, vijiji na kata, huku wakitaka mpango huo uambatane na maboresho ya mfumo wa uondoshaji taka ili kuhakikisha usafi unaofanyika unaendelea kudumu.
Mashindano hayo yamezinduliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bi. Sigilinda Mdemu, wakati wa kikao kazi na Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii, ambapo ameeleza kuwa lengo ni kuongeza ushiriki wa wananchi na viongozi katika kuweka mazingira safi na salama.

Bi. Sigilinda amesema mashindano hayo yanalenga kuongeza hamasa, uwajibikaji na ushindani chanya miongoni mwa mitaa, vijiji na kata, sambamba na kujenga utamaduni wa kufanya usafi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku na kuboresha afya za wananchi.
Hata hivyo, wananchi wamesema mafanikio ya mpango huo yatategemea zaidi namna Halmashauri itakavyoshughulikia changamoto ya taka baada ya wananchi kuzisafisha na kuzikusanya katika maeneo yao.

Mkazi wa Kata ya Kawajense, Mtaa wa Lake View, Justine Joseph, amesema wananchi wamekuwa wakishiriki katika usafi, lakini changamoto hujitokeza katika hatua ya kuondoa taka zilizokusanywa, hali inayoweza kufanya maeneo yaliyosafishwa kurejea kuwa machafu.
Kwa upande wake, mfanyabiashara katika Soko la Matunda la Mtaa wa Lake View, Salma Abubakary, amesema wananchi hukusanya taka wanazozalisha, lakini gari linalohusika na kuziondoa huchelewa kufika, hali ambayo wakati mwingine husababisha taka hizo kuanza kutoa harufu na kuathiri mazingira ya wafanyabiashara na wananchi wanaofika sokoni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wameeleza kuwa mashindano hayo yanaweza kuwa chachu ya kuboresha usafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa, endapo kutakuwa na mfumo unaoeleweka wa ukusanyaji, usafirishaji na utupaji wa taka.
Bi. Sigilinda amewataka Watendaji wa Mitaa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa tozo za huduma za uzoaji taka, akieleza kuwa mapato hayo yanaweza kusaidia kuongeza uwezo wa Halmashauri katika kuboresha huduma ya uondoshaji taka na usafi wa mazingira.
Kwa wananchi, ushindani wa usafi unaonekana kuwa mwanzo mzuri, lakini wanataka hatua hiyo iende sambamba na huduma ya uhakika ya uondoshaji taka, ili usafi wa mitaa, masoko na maeneo ya makazi usibaki kuwa wa mashindano pekee, bali uwe sehemu ya maisha ya kila siku katika Manispaa ya Mpanda.

Discussion
Reader comments
0 contributions