Na Tryphone Odace - Kigoma.
Nyumba mbili zimeteketea kwa moto katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika eneo ya Kilimahewa Kata ya Mwanga Kusini, na Kata ya Bangwe, Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma
Katika matukio hayo, familia mbili zimeachwa bila makazi baada ya nyumba zao kuteketea kwa moto unaodaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme huku mtoto mwenye umri wa miaka miwili akinusurika kifo baada ya nyumba aliyokuwa amelala kuteketea kwa moto.

Waathirika wa matukio hayo akiwemo Christia Lusota wamesema hawakufanikiwa kuokoa mali zilizokuwa ndani ya nyumba hizo, huku wakilalamikia kuchelewa kufika kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
“Nilikuwa nafanya usafi ndani nikasikia harufu ya moto nilivyoenda sebuleni nikakuta moto unawake na tivi na kiti vinawaka moto tukakimbia nje hatujatoa kitu chochote vyote vimeunga lakini tuliwasiliana na Zimamoto lakini hawakuweza kuwahi” amesema Cristia Lusota.
Baadhi ya mashuhuda wamesema walifanya jitihada za kuzima moto huo, lakini hawakufanikiwa kuokoa mali zilizokuwa ndani ya nyumba hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkaguzi Richard Namala, amesema licha ya juhudi zilizofanywa na jeshi hilo, hawakuweza kuokoa nyumba hizo pamoja na mali zilizokuwemo.
“Tumekwamishwa na miundombinu ya barabra na matukio ni mawili kwa wakati mmoja kwa baadhi ya maeneo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuchelewa kufika kwa askari wa zimamoto katika maeneo ya matukio” amesema Richard Namala.
Hata hivyo, Namala amesema hakuna taarifa za majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa kutokana na matukio hayo.
Amewataka wananchi kutumia mafundi wanaotambulika na mamlaka husika wanapohitaji huduma za kuunganisha umeme majumbani, ili kupunguza hatari za hitilafu za umeme na madhara yanayoweza kujitokeza.
Discussion
Reader comments
0 contributions