Na Clavery Christian, Ngara - Kagera.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Karim, amewapongeza viongozi wa CCM Wilaya ya Ngara kwa juhudi walizozionesha katika ujenzi wa ukumbi mkubwa wa chama, akieleza kuwa mradi huo ni ishara ya mshikamano, uzalendo na dhamira ya dhati ya kuimarisha shughuli za chama katika wilaya hiyo.
Karim alitoa pongezi hizo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa ukumbi huo, ambapo alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuwahimiza viongozi pamoja na wanachama kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.

Alisema kukamilika kwa ukumbi huo kutasaidia kuimarisha shughuli mbalimbali za chama pamoja na kutoa mazingira bora kwa ajili ya mikutano na shughuli nyingine za kisiasa na kijamii ndani ya wilaya.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, alizungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Ngara kwa njia ya simu katika kikao kilichowakutanisha makatibu wa CCM wa kata, waenezi wa kata, wenyeviti wa CCM wa kata, makatibu wa jumuiya za kata pamoja na madiwani wa CCM wa wilaya hiyo.

Akizungumza na viongozi hao, Karamagi alisisitiza umuhimu wa umoja, ushirikiano na kujituma katika kutekeleza majukumu ya chama pamoja na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi. Alieleza kuwa CCM inaendelea kuwa chombo muhimu katika kusukuma agenda ya maendeleo kupitia utekelezaji wa sera na mipango inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
“Ni muhimu viongozi katika ngazi zote za chama kuendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa na changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati,” alisema Karamagi.

Aidha, alibainisha kuwa mbunge wa jimbo pamoja na viongozi wengine wa chama wanaendelea kutekeleza wajibu wao kwa kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo na kuharakisha ustawi wa Wilaya ya Ngara.
Kikao hicho kilitumika pia kama fursa ya kujadili mikakati ya kuimarisha shughuli za chama na kuongeza ushiriki wa viongozi na wanachama katika kuhamasisha maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Ngara.

Discussion
Reader comments
0 contributions