Skip to main content

MMOMONYOKO WA MAADILI: WAZAZI, WALEZI WAJIBIKENI KATIKA MALEZI YA WATOTO - SACP JONGO

Na Ibrahim Rojala, Mbogwe - Geita.

MMOMONYOKO WA MAADILI: WAZAZI, WALEZI WAJIBIKENI KATIKA MALEZI YA WATOTO - SACP JONGO

Na Ibrahim Rojala, Mbogwe - Geita.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo, amewataka wazazi na walezi mkoani humo kuwajibika zaidi katika malezi ya watoto wao ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na vitendo vya uhalifu katika jamii.

Akizungumza na wananchi katika mnada wa Ilolangulu, wilayani Mbogwe, SACP Safia amesema changamoto kubwa inayoendelea kuikabili jamii ni kukosekana kwa usimamizi mzuri wa watoto, hali inayowafanya kujiingiza katika mazingira yasiyofaa na kuhatarisha mustakabali wao.

Ameeleza kuwa ni jambo la kawaida kuona watoto wadogo wakizurura maeneo ya masoko hadi nyakati za usiku na wengine wakitumia muda mwingi katika vibanda vya kuonesha sinema bila uangalizi wa wazazi au walezi wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Safia Jongo.

“Changamoto kubwa sana iliyobaki ni malezi ya watoto, Unakuta siku ya soko watoto wadogo mpaka saa nne usiku wanazurura barabarani, Unakwenda kwenye vibanda vinavyoonesha sinema unakuta watoto wadogo wanaangalia sinema hizo, lakini wanaangalia nini? Kitu hicho kinamfundisha nini?” amesema SACP Safia.

Kwa mujibu wa RPC Safia, hali hiyo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa vitendo vya mmomonyoko wa maadili pamoja na matukio ya ukatili dhidi ya watoto.

Katika hatua nyingine, SACP Safia Jongo amewataka watumishi wa umma kutumia taaluma zao kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi, akisisitiza kuwa maendeleo ya wananchi yana mchango mkubwa katika kupunguza vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama.

Amesema kila mtumishi wa serikali anapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki zinazolenga kuleta maendeleo katika maeneo yao.

“Usalama utakuwa mzuri zaidi kama kila mmoja wetu kwenye nafasi yake atatekeleza wajibu wake,Mtendaji wa kata ahakikishe anawasaidia wananchi kutatua changamoto zao kwa kuwasaidia wananchi yale matatizo ambayo serikali iliona ikulete huku,lakini pia wewe afisa mifugo unashirikiana vipi na wafugaji wa kata ya Ilolangulu kuhakikisha kwamba wanapata maendeleo”ameeleza

Aidha, amewataka maafisa maendeleo ya jamii (Mabibi na mabwana Maendeleo) kuwasaidia vijana na wanawake kubuni na kuanzisha miradi ya maendeleo pamoja na kuwawezesha kupata mikopo inayotolewa na serikali, hatua itakayosaidia kupunguza ukosefu wa ajira na vitendo vya uhalifu.

Wakati huo huo, SACP Safia Jongo amewataka wananchi mkoani Geita kutokubali kutoa rushwa katika upatikanaji wa huduma za kipolisi, akisisitiza kuwa huduma zote zinazotolewa na Jeshi la Polisi ni bure.

“Huduma zote za kipolisi ni bure, marufuku kuombwa au kutoa fedha kwa ajili ya huduma za kipolisi. Usikubali kutoa pesa kwa ajili ya dhamana wala kwa ajili ya kukamatwa au kuachiwa mtuhumiwa,” amesema.

Amehimiza wananchi kutoa taarifa wanapokutana na vitendo vya rushwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Kauli za SACP, Safia Jongo huyo zinakuja wakati serikali na wadau mbalimbali wakiendelea kuhimiza ushiriki wa jamii katika malezi ya watoto, kukuza maadili mema na kuimarisha usalama wa wananchi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.