Skip to main content

MKONGWE WA MAIGIZO EVA MARIE SAINT AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 102

Muigizaji mkongwe wa Marekani na mshindi wa tuzo ya Oscar, Eva Marie Saint, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 102 akiacha historia kubwa katika tasnia ya filamu baada ya zaidi ya miongo saba ya kazi yake iliyomfanya kuwa miongoni mwa nyota mashuhuri wa kizazi cha dhahabu cha Hollywood.

MKONGWE WA MAIGIZO EVA MARIE SAINT AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 102
Studio Narration JAMBO FM

MKONGWE WA MAIGIZO EVA MARIE SAINT AFARIKI DUNIA AKIWA NA MI...

0:00 --:--

Muigizaji mkongwe wa Marekani na mshindi wa tuzo ya Oscar, Eva Marie Saint, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 102 akiacha historia kubwa katika tasnia ya filamu baada ya zaidi ya miongo saba ya kazi yake iliyomfanya kuwa miongoni mwa nyota mashuhuri wa kizazi cha dhahabu cha Hollywood.

Saint amefariki Jumanne nyumbani kwake jijini Los Angeles kutokana na sababu za asili akiwa amezungukwa na familia na wapendwa wake kwa mujibu wa mwakilishi wa familia yake, Jeff Sanderson.

Kifo chake kimemfanya kuwa mmoja wa mastaa wa mwisho wa kizazi cha zamani cha Hollywood na wakati wa kifo chake alikuwa pia ndiye mshindi wa Oscar aliyekuwa akiishi kwa umri mkubwa zaidi.

Safari yake ya umaarufu ilianza kwa kishindo mwaka 1954 kupitia filamu On the Waterfront, iliyoongozwa na Elia Kazan.

Hiyo ilikuwa filamu yake ya kwanza kabisa lakini badala ya kuwa mwanzo wa kawaida wa safari yake Saint alifanya historia kwa kushinda tuzo ya Academy Award ya Mwigizaji Bora Msaidizi kutokana na uigizaji wake wa Edie Doyle, mhusika aliyekuwa mpenzi wa mhusika aliyeigizwa na Marlon Brando.

Uhusiano wake wa kikazi na Brando ulikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya filamu hiyo. Brando alikuwa maarufu kwa uigizaji wa aina ya method acting, jambo lililomfanya Saint kuvutiwa lakini pia kuhisi hofu kidogo alipokuwa akifanya kazi naye.

Katika mahojiano yake ya mwaka 2013 na Turner Classic Movies Saint aliwahi kueleza kuwa Brando alikuwa mtu aliyemfanya ahisi kana kwamba angeweza kuona kila kitu ndani yake.

Miaka mitano baadaye, Saint aliongeza filamu nyingine kubwa kwenye historia yake alipocheza nafasi ya Eve Kendall katika North by Northwest, filamu ya mwaka 1959 iliyoongozwa na mmoja wa waongozaji wakubwa wa wakati wote Alfred Hitchcock.

Katika filamu hiyo alicheza pamoja na Cary Grant na kuigiza mwanamke mwenye siri ambaye anajikuta katika mazingira hatari ya upelelezi na kusafiri.

Uigizaji wake katika North by Northwest ulimfanya kuwa sehemu ya kundi maarufu la waigizaji wanawake waliowahi kufanya kazi na Hitchcock.

Saint alieleza kuwa Cary Grant alikuwa makini sana katika kumtengenezea taswira ya mhusika wake, kuanzia nywele, makeup, viatu, vito, pochi hadi glavu.

Kwa Saint mchakato huo ulimsaidia kuelewa zaidi mhusika wa mwanamke wa upelelezi aliyekuwa akimuigiza.

Baada ya mafanikio hayo, Saint aliendelea kuonekana katika filamu mbalimbali kubwa.

Mwaka 1960 aliigiza pamoja na Paul Newman katika Exodus, huku baadaye akionekana katika All Fall Down ambako alicheza pamoja na Warren Beatty.

Hata hivyo tofauti na mastaa wengi waliokuwa wakitafuta kuendelea kuwa kwenye kilele cha umaarufu, Saint alianza kujiondoa taratibu katika mwangaza wa Hollywood ili kujikita zaidi katika maisha ya familia.

Aliolewa na mwongozaji Jeffrey Hayden na ndoa yao ilidumu kwa miaka 65 hadi kifo cha Hayden mwaka 2016.

Wawili hao walipata watoto wawili. Saint aliwahi kueleza kuwa kuondoka kwake kwa muda katika mwangaza wa Hollywood kulihusiana kwa kiasi kikubwa na uamuzi wake wa kulea familia.

Licha ya kuwa mbali na Hollywood kwa muda mrefu, Saint alifanya comeback kubwa kwenye sinema miaka kadhaa baadaye.

Akiwa tayari katika miaka yake ya 80, alirejea kwenye filamu kubwa Superman Returns ya mwaka 2006, ambako alicheza nafasi ya Martha Kent, mama mlezi wa Superman. Kurudi kwake kulionyesha kuwa kipaji chake bado kilikuwa na nafasi katika kizazi kipya cha filamu.

Baada ya hapo aliendelea kupata nafasi nyingine katika filamu, akiwemo Winter's Tale, ambako alicheza pamoja na Colin Farrell na Russell Crowe, pamoja na Mariette in Ecstasy ya mwaka 2019.

Pia aliwahi kushinda Emmy mwaka 1990 kutokana na uigizaji wake katika miniseries People Like Us, hivyo mafanikio yake hayakuishia kwenye filamu pekee bali pia yalifika katika televisheni.

Katika maisha yake yote ya sanaa, Eva Marie Saint alitunukiwa pia nyota mbili kwenye Hollywood Walk of Fame, heshima inayoonyesha mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani nchini Marekani.

Saint aliwahi kusema kuwa kuishi kwa muda mrefu na kupitia uzoefu mbalimbali wa maisha kulimsaidia kuwa mwigizaji bora zaidi.

Kwake, kadiri mtu anavyoishi muda mrefu ndivyo anavyopata uzoefu mwingi wa kihisia na kuelewa zaidi maisha ya watu wengine, jambo aliloamini lilimsaidia katika kuigiza wahusika wake.

Eva Marie Saint ameondoka duniani akiwa na umri wa miaka 102, lakini ameacha urithi ambao unaanzia kwenye filamu za Hollywood za miaka ya 1950 hadi sinema za karne ya 21.

Kutoka On the Waterfront hadi North by Northwest na Superman Returns, jina lake limebaki sehemu ya historia ya Hollywood na kizazi cha waigizaji kilichobadilisha sura ya sinema duniani.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.