Skip to main content

MKOA WA KIPOLISI TARIME-RORYA WAENDELEZA UKAGUZI MABASI YA SHULE, WATOA ELIMU

Na Adam Msafiri - Mara.

MKOA WA KIPOLISI TARIME-RORYA WAENDELEZA UKAGUZI MABASI YA SHULE, WATOA ELIMU

Na Adam Msafiri - Mara.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya limesema linaendelea na ukaguzi wa mabasi ya shule pamoja na kutoa elimu kwa madereva na wahudumu wa wanafunzi ili kuhakikisha usalama wa watoto unazingatiwa kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula ujao.

Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa magari ya shule lililofanyika mjini Tarime mkoani Mara, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mark Njera amesema kufanya ukaguzi huo kipindi cha likizo kunatoa nafasi kwa wamiliki wa magari kufanya matengenezo na kurekebisha kasoro zitakazobainika kabla ya wanafunzi kurejea shuleni.

Amesema lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha magari yote yanayotarajiwa kutumika kusafirisha wanafunzi yanakuwa katika hali nzuri, yanakidhi matakwa ya sheria za usalama barabarani na yanabeba idadi ya wanafunzi inayoruhusiwa kwa mujibu wa uwezo wa gari husika.

Njera pia amewataka madereva na wamiliki wa mabasi ya shule kuzingatia sheria zote za usalama barabarani na kuhakikisha wanafunzi wanasafirishwa katika mazingira salama wakati wote.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya, Kamanda Hamis Wembo amesema zoezi hilo limekuwa pia fursa ya kutoa elimu kwa madereva na wahudumu wa wanafunzi kuhusu wajibu wao wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, unyanyasaji na mazingira yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Amesema wahudumu wa wanafunzi katika mabasi ya shule wana nafasi muhimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wa safari na kwamba wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuripoti viashiria vyovyote vya ukatili au unyanyasaji.

Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Magari ya Shule Tarime, Tumaini Abel, pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Shule Binafsi Tarime, Happiness Winani, wamepongeza hatua hiyo ya Jeshi la Polisi wakisema itasaidia kuongeza usalama wa wanafunzi na kuboresha huduma za usafiri wa shule wilayani humo.

Naye muhudumu wa wanafunzi, Jenny Nicodemo, amesema elimu iliyotolewa imewasaidia kuelewa zaidi wajibu wao katika kulinda usalama na ustawi wa watoto wanaowahudumia wakati wa safari za kwenda na kurudi shuleni.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.