Na Saulo Stephen - Singida.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga ameshiriki zoezi la utiaji saini mikataba ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Makazi ya wakuu wa Wilaya na nyumba ya Katibu Tawala wa Mkoa na Makampuni yatakayohusika.
Hayo yamejiri katika Ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida yakishuhudiwa na wajumbe wa Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Singida ambapo makampuni sita(6) yameshiriki utiaji saini mikataba hiyo itakayowawezesha kuanza kazi mara moja.

Mkoa wa Singida ulipokea fedha kutoka Serikali kuu ikiwa ni kiasi cha Shilingi Bilioni moja kwa kila Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba,Singida na Manyoni,kiasi cha shilingi 454,281,000 kujenga makazi ya viongozi wa wilaya hizo huku nyumba ya Katibu Tawala wa Mkoa ikitengewa kiasi cha shilingi Milioni mia tano(500,000,000).
Ujenzi wa ofisi za Wakuu wa Wilaya pamoja na nyumba zao za kuishi unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na utendaji wa serikali kwa ujumla ikiwemo huduma za kiutawala kusogezwa karibu zaidi na wananchi, hivyo kupunguza muda na gharama za kufuatilia huduma mbalimbali.

Aidha, uwepo wa ofisi za kudumu utasaidia kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo kama vile barabara, elimu na afya, kwa kuwa viongozi watakuwa na mazingira bora ya kufanya kazi. Hali hii pia itaongeza uwajibikaji kwa viongozi, kwani wananchi watakuwa na nafasi rahisi ya kufika ofisini, kutoa maoni yao na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya serikali.
Discussion
Reader comments
0 contributions