Na Saulo Stephen - Singida.
Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, imesema itaendelea kuwekeza katika miradi ya elimu, afya na miundombinu katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya wilaya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Wilayani Mkalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Hajjati Asia Messos, amesema miongoni mwa miradi itakayotekelezwa ni ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Ishenga kupitia mradi wa SEQUIP, ukamilishaji wa maabara, madarasa, nyumba ya mwalimu, mabweni, vyoo pamoja na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA katika shule mbalimbali.
Mbali na sekta ya elimu, amesema halmashauri itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na vituo vya afya vya Ilunda na Gumanga, huku pia ikijenga nyumba tatu za wakuu wa idara ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.

Bi. Hajjati amesema halmashauri itaendelea kuweka kipaumbele katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia sekta za kilimo, mifugo, afya na elimu ili kuongeza ustawi wa wananchi.
Aidha, amewashukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo, huku akiwapongeza watumishi wa halmashauri, Baraza la Madiwani na wananchi wa Mkalama kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia amewahimiza wananchi kuendelea kulinda amani na kushirikiana na vyombo vya serikali kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu, huku akiwataka watumishi wa umma kuongeza uwajibikaji, ubunifu na kasi ya utendaji kazi ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Discussion
Reader comments
0 contributions