Skip to main content

MKAKATI: MIAKA MITANO KUKOMESHA VITENDO VYA UKEKETAJI SINGIDA

Na Saulo Stephen – Singida.

MKAKATI: MIAKA MITANO KUKOMESHA VITENDO VYA UKEKETAJI SINGIDA

Na Saulo Stephen – Singida.

Vitendo vya ukeketaji, vimeendelea kuwa changamoto inayogusa maisha, afya na mustakabali wa watoto wa kike, huku Mkoa wa Singida ukianza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukomesha na Kutokomeza Ukeketaji kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 hadi 2029/2030.

Mpango huo, unalenga kuhusisha wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya ukeketaji, kwa kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu kwa jamii, ulinzi wa mtoto na ushirikishwaji wa viongozi wa kimila, viongozi wa dini pamoja na wazazi.

Kwa miaka mingi, ukeketaji umekuwa ukifanyika katika baadhi ya jamii kama sehemu ya mila na desturi, lakini madhara yake kwa watoto wa kike yameendelea kuibua hofu na wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kuutokomeza.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago.

Akizungumza na Jambo Media kuhusu mpango huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago, amesema Mkoa umejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu dhidi ya ukeketaji inawafikia wananchi na jamii inaelewa madhara yanayotokana na vitendo hivyo.

Mbago amesema, ushirikishwaji wa viongozi wa kimila, viongozi wa dini, wazazi na walezi ni muhimu katika kuhakikisha mapambano hayo yanafanikiwa, kwa kuwa viongozi hao wana nafasi kubwa katika kubadili mitazamo na mila zinazoweza kuwaweka watoto wa kike katika hatari.

Kwa upande wa watoto wa kike, wameendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi kuwalinda na kuacha kuwafanyia vitendo vya ukeketaji, wakieleza kuwa wanahitaji kukua katika mazingira salama na kupata haki zao za msingi bila kufanyiwa vitendo vinavyoweza kuhatarisha afya na maisha yao.

Mmoja wa wanawake aliyefanyiwa ukeketaji akiwa mtoto ameeleza madhara aliyokutana nayo kutokana na kitendo hicho, akitoa wito kwa jamii kuachana na ukeketaji na kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi ya mila na desturi zenye madhara.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukeketaji ni Arusha kwa asilimia 43, ikifuatiwa na Manyara kwa asilimia 28, huku Mkoa wa Singida ukishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.

Takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa changamoto hiyo na umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja katika kutoa elimu kwa jamii, kuwalinda watoto na kuhakikisha mifumo ya kuzuia na kukomesha vitendo vya ukeketaji inafanya kazi kwa ufanisi.

Wadau wa mapambano dhidi ya ukeketaji wamesisitiza umuhimu wa jamii kubadili mitazamo na kuachana na mila zinazoweza kuhatarisha afya na maisha ya watoto wa kike.

Kwa Mkoa wa Singida, utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitano unalenga kuleta mabadiliko katika jamii na kuhakikisha kizazi kijacho cha watoto wa kike kinakua bila kukabiliwa na ukeketaji na madhara yanayotokana na vitendo hivyo.

Mapambano dhidi ya ukeketaji yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja, kwani kulinda mtoto wa kike si jukumu la mzazi pekee, bali ni wajibu wa familia, jamii, viongozi wa kimila na dini pamoja na serikali.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.