Na Gideon Gregory - Dodoma.
Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, unatarajiwa kuingia hatua mpya ya maendeleo Septemba 8, 2026 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuzindua majengo ya ofisi za Wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na kilomita 57.1 za barabara za lami.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 06,2026 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi amesema uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji huo ni hatua muhimu katika kuimarisha Dodoma kama kitovu cha shughuli za Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.
"Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda yaliyoanza kujengwa Novemba 28, 2018 na kukamilika Machi 22, 2019, majengo hayo yaliwezesha baadhi ya watumishi wa Serikali kuhamia Mtumba wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya ujenzi wa majengo ya kudumu," amesema.

Amesema awamu ya pili ilianza Oktoba 2021 na kuhusisha ujenzi wa majengo ya kudumu pamoja na miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.
"Mbali na barabara, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42, mifumo ya maji safi na maji taka, TEHAMA, mifumo ya usalama ya CCTV, vituo vya zimamoto pamoja na shughuli za upandaji miti na uendelezaji wa mandhari ya mji,"amesema.
Pia ameongeza kuwa majengo hayo yamebuniwa kwa aina nne kulingana na mahitaji ya watumishi ambapo baadhi yana uwezo wa kuchukua watumishi 300, mengine 500, huku jengo kubwa likiwa na uwezo wa kuchukua hadi watumishi 1,400.

Kwa upande mwingine uwekezaji huo unaonekana kuwa na umuhimu mpana kwa Dodoma, kwa kuwa shughuli za Serikali zinapoongezeka mahitaji ya usafiri, biashara, huduma na makazi nayo huongezeka.
Hivyo uzinduzi wa Septemba 8, 2026 unakuja kama alama nyingine katika safari ya kuindeleza Dodoma na kuifanya kuwa mji unaokidhi mahitaji ya Serikali na wananchi katika mazingira ya kisasa.
Discussion
Reader comments
0 contributions