Na Daniel Gahu - Katavi.
Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya elimu nchini baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mpimbwe yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 342 na kuzindua rasmi bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Usevya lenye thamani ya shilingi milioni 136, wilayani Mpimbwe, mkoani Katavi.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe. Nanauka amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata mazingira bora, salama na rafiki ya kujifunzia, yatakayochochea ufaulu na kujenga msingi imara wa maendeleo ya taifa.

"Serikali imejipanga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata haki ya elimu bora. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika ujenzi wa shule na miundombinu ya elimu ili kuwaandaa watoto wetu kuwa taifa lenye maarifa na ushindani," amesema Mhe. Nanauka.
Ameeleza kuwa juhudi hizo hazilengi maeneo ya mijini pekee, bali zinahusisha pia maeneo ya vijijini na pembezoni ili kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za elimu bila kujali mahali wanapoishi.

Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka amezindua bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Usevya, akisema mradi huo utasaidia kuboresha mazingira ya kuishi na kujifunza kwa wanafunzi, kuongeza utulivu wa masomo na kuchangia kuimarika kwa matokeo ya kitaaluma.
"Maendeleo ya elimu hayaishii kwenye madarasa pekee. Tunahitaji pia mazingira salama na rafiki ya kuishi kwa wanafunzi ili waweze kujifunza kwa utulivu na kufikia ndoto zao," amesisitiza.

Akihitimisha ziara yake, Mhe. Nanauka ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo, akibainisha kuwa ubora wa ujenzi unaakisi matumizi sahihi ya fedha za umma na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha huduma za elimu kwa wananchi.
Ujenzi wa Shule ya Msingi Mpimbwe pamoja na bweni la wavulana la Shule ya Sekondari Usevya unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za elimu, kupunguza changamoto za miundombinu na kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kufikia malengo yao ya kielimu.


Discussion
Reader comments
0 contributions