Na Gideon Gregory - Dodoma.
Serikali imesema jumla ya shilingi billioni 1 zimetengwa katika mwaka wa fedha wa 2026/27 kwa ajili ya kuendelea kuongeza miundombinu mipya kwenye Hospitali ya Wilaya ya Meatu ambapo itajenga jengo la Wazazi, kumalizia jengo la maabara, kujenga walkway na kujenga visima vya kukusanya maji ya mvua.
Hayo yameelezwa leo Mei 25, 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Meatu Mhe.Salum Khamis Salum aliyehoji ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Meatu.
Dkt. Dugange amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Hospitali ya Meatu mpaka miundombinu yote muhimu kwenye hospitali hiyo itakapokamilika.

"Hospitali ya wilaya ya Meatu ilipandishwa hadhi kutoka kituo cha afya mwaka 1977. Baada ya Kituo hiki kupandishwa hadhi, Serikali imeendelea kupeleka fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa lengo la kuongeza miundombinu ya Hospitali hiyo ili iendane na mahitaji ya sasa,"amesema
Amesema katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilipeleka shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara na nyumba ya mtumishi.
"Katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2023/24 Serikali ilipeleka shilingi bilioni 1.15 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kutolea hudumu mbalimbali za afya ambayo ujenzi wake umeshakamilika," amesema.
Discussion
Reader comments
0 contributions