Na Ibrahim Rojala - Geita.
“Tangu tukiwa wadogo tulimuona mama akishona mpaka tulipokuwa watu wazima, kwahiyo baada ya kumaliza chuo nikawa nimeajiriwa,nikawa nafanya kazi na biashara yangu ya ushonaji ambapo mama ndiye alikuwa fundi mkuu msimamizi,lakini baadae nikaamua kuachana na ajira na kubase moja kwa moja kwenye kazi yangu ya ubunifu wa mitindo.”
Ni sehemu tu ya baadhi ya yaliyoelezwa na Bertha Joseph Komba, mbunifu wa mitindo mbalimbali ya mavazi ambaye umaarufu wake umebebwa na jina la Kasikana Designer, kiwanda chake cha Kasikana Clothing Factory kikiwa ndani ya Manispaa ya Geita Mkoani Geita.
Wazo la Utimizaji ndoto Lilioanzia Nyumbani
Akisimulia msingi wa mafanikio yake kupitia ubunifu wa mitindo ya mavazi kamwe hasahau mchango wa familia yake kutokana na ukweli kwamba wazo la uanzishwaji wa safari hiyo ya mafanikio lilianzia ndani ya familia, kutoka kuutumia ufundi ushonaji wa mama yake mzazi hadi kumiliki kiwanda kinachozalisha mavazi ya mitindo ya mataifa mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko.

Lakini Kama ambavyo nyakati nyingine ili jambo moja kutokea ni lazima lingine life,hali hii pia ilitokea kwa Bertha kwani muda haukumtosha na alihitajika kazini katika wakati ambao pia alihitaji kutimiza ndoto zake kupitia ubunifu wa mitindo ya mavazi,ndipo alipoamua kuchagua moja,kuacha kazi na kuamua kuipambania ndoto yake.
Lakini uamuzi wa kuacha kazi pekee haukutosha kwani utafiti alioufanya kwa kipindi cha miaka mitatu kati ya 2018 hadi 2020 ulimuonesha kuwa kuna fursa mkoani Geita, hivyo alipaswa kuiacha Dar Es Salaam, jiji la ndoto za wengi na kuhamia mmkoani Geita na moja kati ya silaha muhimu ya kibiashara aliyoamua kuitumia ilikuwa ni kujitofautisha na wengine kwa kujikita katika mambo makuu mawili.
Mosi ilikuwa ni kubuni na kushona mitindo ya mbalimbali ya nguo na kuziuza dukani kwake na pili ni kwa wateja kuwa na chguo la kufika kiwandani,kuchagua aina ya mitindo wanayohitaji na kushonewa kulingana na mahitaji yao.
“Hii ilikuwa tofauti na namna nilivyokuwa nikifanya Dar Es Salaam kwani huko walengwa wangu walikuwa wasanii na wafanya maonesho ya mitindo ya mavazi majukwaani,” anasema Bertha.

Changamoto ya Bei na Msimamo wa Kutoshusha Thamani
Safari ya kuzifia ndoto za kuupeleka ubunifu wa Mavazi kimataifa akiwa mkoani Geita mwanzoni haikuwa rahisi hata kidogo kwani waliolengwa na ubunifu wake kila walipogusa bidhaa zake walitoa milio! Likuwa ikuhusu bei za bidhaa ambazo katika kipindi ambacho yeye aliona amezipunguza, wateja waliona ni kama wanaibiwa na hata alipojaribu kupunguza tena mambo yakawa magumu.
“Nikaona kidogo nireduce price zangu,kwahiyo nikafanya hivyo lakini bado ikawa mtu ukimtajia price anaacha mdomo wazi,nikasema msimamo wangu ni huo kwamba sitashusha bei,wakwangu ambao Mungu ameniapngia watakuja tu,watakaoona wanafaa kwenda kwenye bai za jioni well and good waende”anasimulia Kasikana Designer.
Hapa ni kama aliamua kusimamia mtazamo wa Ralph Waldo Emerson mwanafalsafa, mwandishi wa insha, na mshairi mashuhuri wa Marekani ambaye alikuwa mwanzilishi mkuu wa harakati ya kifalsafa na kiutamaduni iliyojulikana kama Transcendentalism (Falsafa ya Upitaji Mipaka) wakati akizungumzia kujitegemea alisema, “Kuwa wewe mwenyewe katika dunia inayojaribu kila mara kukufanya uwe mtu mwingine, ni moja ya mafanikio makubwa zaidi.”

Kasikana Designer anaeleza kwamba hali ilikuwa mbaya zaidi kiasi kwamba ilifika mahali makasiriko yalijitokeza hadharani na hata kujadiliwa kuwa anajifanya mbunifu wa gharama kubwa,lakini aliongozwa na jambo moja pekee,dhamira ya ndani ambayo ilikuwa ni kujitofautisha na kutoa maana halisi ya tofauti iliyopo kati ya mbunifu na fundi wa kawaida.
Teknolojia Kama Sehemu ya Biashara
Maendeleo ya Teknolojia chanuo Kasikana aliiona kuwa ni fursa mpya ya kulifikia soko la ndani na nje ya nchi kwa urahisi hivyo ameamua kuifanya Teknolojia kuwa sehemu ya maisha yake kwa kuweka kanuni mbalimbali katika matumizi ya Teknolojia.
Kanuni yake ya kwanza ni bora kutochapisha chochote katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kuliko kupandisha picha mnato au picha mjongeo za kazi zisizo na ubora.

“Maendeleo ya Teknolojia kwa upande wangu nimeyachukulia very serious kiasi ambacho nimeweza kushiriki hata kweny baadhi ya short courses mbalimbali, nimeweza kwenda hadi India kusomea jinsi ya kutengeneza maudhui yaani Media Content Generation Using Latest Tools, pia nina uelewa mkubwa wa matumizi ya Teknolojia katika kuisukuma biashara yangu kwenda mbali zaidi”anasema
Katika eneo hili la Teknolojia anaeleza kwamba dhamira yake ni kutaka kujifunza kila siku akieleza kuwa hatua hiyo inatokana na kuona matokeo chanya ya matumizi ya mitandao ya kijamii katika biashara zake.
Mafanikio Yanayozalisha Fursa Kwa Wengine
Kasikana Clothing Factory sio tu kwamba imekuwa na mafanikio kwa mmiliki pekee,imekuwa chanzo cha ajira kwa mafundi wanaoingia na kutoka kila wakati katika kiwanda hicho,wakiacha na kuchukua bunifu mbalimbali ambazo wakati mwingine huenda nazo kwa wabunifu mbalimbali wa mitindo ya mavazi hapa nchini.

Kutenganisha Majukumu ya Kazi Na Familia
“Moyo wangu ni kama nyumba ilivyo na vyumba, nimeugawa katika vyumba pia,kuna chumba cha kazi,chumba cha familia na chumba cha mambo mengineyo,kwahiyo watoto wangu wanajua kuwa hii ni sehemu ya kazi ambayo pia ndio chanzo kukii cha kipato,ada nakadhalika hivyo wanaelewa ingawa wakati mwingine ninapokuwa nina safari nyingi huwa nawakumbuka sana”anasema Kasikana Designer
Miaka 14 ya Kujifunza, Kupambana Na Kukua
Usiku unapokuwa mkubwa ni dalili ya kuwa kunakaribia kupambazuka,baada ya muda kitambo kupita somo likawaingia wateja na wakaelewa namna ya kutofautisha kati ya mitindo ya mavazi yenye matokeo ya ubunifu ndani yake na mavazi yanayolenga kusitiri mwili pekee na hili liliwezekana baada ya wateja kuzoea hali halisi na funzo katika hili ni kuwa msimamo ni muhimu katika kila jambo.
Hii ni safari ya miaka 14 ya kupanda na kushuka kwa chanuo Kasikana Designer ambaye anaeleza kwamba katika kipindi chote hicho lichay achangamoto mbalimbali kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuweza kuwa na mtandao mkubwa wa ushirikiano na wabunifu wa mitindo ya mavazi ndani ya nchi,afrika na nje ya bara la Afrika.

Tuzo Kama Alama ya Mafanikio ya Safari
Ndani ya kipindi hicho pia anasema ameweza kujifunza mambo mengi nyanayohusu ubunifu katika nchi mbalimbali kutokana na kujijengea utamaduni wa kutembelea wabunifu wengine katika nchi mbalimbali na kwake juhudi zimezaa matunda kwa kumtambulisha katika majukwaa mbalimbali ya Kimataifa.
Hilo linajidhihirisha kutokana na ukweli kwamba hadi sasa amefanikiwa kutwaa tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ambazo ni ishara ya utambuzi wa mchango wak katika sekta ya mavazi na ubunifu kama vile tuzo ya Khimji’s Upcoming Designer of The Year aliyoipata mwaka 2017 kupitia Jukwa la Swahili Fashion Week ikiwa ni tuzo yake ya kwanza tangu alipoanza kazi za ubunifu.
Katika kumbukumbu zake pia ana tuzo ya East African Celebrity Designer Of The Year ya mwaka 2022-2023, Tuzo ya African Female Influencer Of The Year, Top 100 African’s Global iliyolenga kutambua jitihada za uinuaji wa biasahara ndani na nje ya nchi aliyoipata mwaka 2026 na pia ni mshindi wa Tuzo ya Malikia wa dhahabu, kipengele cha Kiongozi Bora katika Sekta binafsi aliyoshinda mwaka 2026.

Ndoto ya Kuajiri Zaidi ya Watu 200
Licha ya Mafaniko yaliyopatikana, malengo ya juu zaidi bado yapo, shauku ya Bertha Kasikana ni kuona kiwanda chake kikikua zaidi ndani ya miaka mitatu ijayo na kuwa na uwezo wa kuajiri mafunzi zaidi ya 200 kwa wakati mmoja, kuzalisha bidhaa kwa kiwango kikubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuzalisha jozi 1000 za mavazi kwa wakati mmoja, hapa ikiwa imelengwa migodi mikubwa ya uchimbaji wa madini.
Lengo lingine ni kuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua tenda kwa taasisi zenye idadi kubwa ya wafanyakazi, kuvalisha makundi makubwa ya watu katika matukio mbalimbali ya kijamii na yenye uhitaji wa sare nyingi.

Kutoka kwenye cherehani ya mama hadi kiwanda, Safari ya Kasikana Designer kuipata Kasikana Clothing Factory kutimiza ndoto kupitia ubunifu inaubeba msemo wa aliyekuwa mvumbuzi, mwekezaji, na mfanyabiashara mkubwa wa Marekani ambaye alikuwa mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mkuu wa Apple Inc, Steve Jobs.
Jobs aliwahi kusema “You've got to find what you love”(Unatakiwa Kutafuta Unachokipenda) kupitia hotuba yake maarufu aliyoisoma mnamo Juni 12, 2005 katika chuo kikuu cha Stanfordkupitia Hotuba hiyo Steve Jobs alieleza namna alivyoacha masomo katika liacha Chuo cha Reed (Reed College) kwa sababu hakuona thamani ya kuendelea na masomo na badala yake kuchagua alichokipenda.
Baada ya kuacha, aliendelea kubaki chuoni hapo na kuhudhuria masomo huru aliyoyapenda kama vile ya uandishi wa mitindo ya maandishi (calligraphy), ambayo baadaye yalimsaidia sana katika kubuni miandiko mizuri ya kompyuta za Mac na simu za iPhone, Kasikana Designer pia aliacha ajira na kuchagua anachokipenda.
Kutoka kwenye cherehani aliyokuwa akimuona mama yake akiitumia akiwa mtoto, hadi kwenye kiwanda kinachobeba ndoto ya kuajiri mamia ya watu, safari ya Bertha Komba, maarufu kama Kasikana Designer, inaonesha kuwa ndoto hazitimii kwa kuzitamani pekee, bali kwa kuthubutu kuzifanyia kazi hata pale mazingira yanapolazimisha mtu kubadilika.
Discussion
Reader comments
0 contributions