Na Tryphone Odace - Kigoma.
Halmashauri ya Wilaya Kakonko Mkoani Kigoma, imesema miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali imeendelea kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Kakonko.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli, amesema Halmashauri hiyo itaongeza kasi ya utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027, hususan ujenzi wa vyoo vya shule ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Aidha, amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanafyatua matofali kabla ya Septemba 2026 ili kuwezesha utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa wakati.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Fidel Chiza Nderego, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuielekezea wilaya hiyo miradi mbalimbali ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.

“Tuendelee kushirikiana na wananchi kwa kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza miradi hiyo ambayo serikali imeleta katika wilaya yetu ili ilete manufaa endelevu kwa jamii” amesema Stephano Ndaki Mhuli.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, amesema Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kupitia uwekezaji katika ujenzi wa Ofisi za TFS, vituo vya Polisi pamoja na kuimarisha huduma za Zimamoto, Uhamiaji, TANESCO na RUWASA. Amesema hatua hizo zinachangia kuimarisha usalama, upatikanaji wa huduma bora na ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Kakonko.

Viongozi waliohudhuria Baraza hilo wamehimiza kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa wananchi ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaendelea kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Wilaya ya Kakonko.
Discussion
Reader comments
0 contributions