Skip to main content

MIRADI YA KIMKAKATI MUSOMA IMEKIDHI VIWANGO - MHA. MATIVILA

Na Adam Msafiri, Musoma - Mara.

MIRADI YA KIMKAKATI MUSOMA IMEKIDHI VIWANGO - MHA. MATIVILA

Na Adam Msafiri, Musoma - Mara.

Ubora wa miradi ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 19.9 inayotekelezwa katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara umethibitishwa baada ya vipimo vya maabara kuonyesha kuwa kazi zinazofanyika zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo pamoja na kushuhudia vipimo vya ubora wa vifaa vya ujenzi katika maabara.

Mhandisi Mativila amesema matokeo ya ukaguzi yanaonyesha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kwamba serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Nyabiti, amesema tathmini hiyo imeondoa mashaka yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya wananchi kuhusu kiwango cha ubora wa miradi inayotekelezwa katika manispaa hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Bweri, Paul Katikilo, amepongeza hatua ya serikali kufanya ukaguzi wa moja kwa moja wa miradi hiyo ikiwemo mradi wa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi mjini Musoma kinachojengwa katika kata ya Bweri, akieleza kuwa wananchi sasa wamepata uhakika kuhusu ubora wa kazi zinazoendelea.

Afisa wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Mudy Itanga, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na hatua mbalimbali zimefikiwa kulingana na ratiba iliyowekwa.

Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Shaaban, Mkendo na Musoma Bus–Saa Nane, jengo la ofisi, stendi ya mabasi ya Bweri pamoja na Soko la Nyasho. Miradi hiyo inatekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 19.9.

Ukaguzi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini inazingatia viwango vya ubora na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.