Skip to main content

MILIONI 256 ZA MIKOPO ISIYO NA RIBA KUYANUFAISHA MAKUNDI MBALIMBALI BUKOMBE

Na Ibrahim Rojala, Bukombe - Geita.

MILIONI 256 ZA MIKOPO ISIYO NA RIBA KUYANUFAISHA MAKUNDI MBALIMBALI BUKOMBE
Studio Narration JAMBO FM

MILIONI 256 ZA MIKOPO ISIYO NA RIBA KUYANUFAISHA MAKUNDI MBA...

0:00 --:--

Na Ibrahim Rojala, Bukombe - Geita.

Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 256 kwa ajili ya utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu katika robo ya nne ya mwaka wa fedha.

Akizungumza katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dkt. Doto Biteko, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erick Kagoma amesema, fedha hizo zitatolewa kwa vikundi vitakavyokidhi vigezo baada ya kufanyiwa tathmini na wataalamu wa halmashauri.

Kagoma amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga katika vikundi na kuomba mikopo hiyo ili waweze kunufaika nayo na kukuza uchumi wa familia zao.

Amebainisha kuwa lengo la mikopo hiyo ni kuwawezesha kiuchumi makundi maalum na kuinua kipato chao.Aliongeza kuwa mapema mwaka huu, halmashauri ilitoa zaidi ya shilingi milioni 196 kwa vikundi 26, hatua iliyowezesha wanufaika kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola, amempongeza Mbunge Dkt. Biteko kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo, akieleza kuwa utekelezaji wa miradi unaendelea vizuri kutokana na upatikanaji wa fedha kutoka serikalini.

Kwa upande wake, Dkt. Biteko amewataka wananchi na wanachama wa CCM kutumia fursa ya mikopo hiyo isiyo na riba ili kubadili maisha yao. Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Bukombe ni miongoni mwa halmashauri zinazoongoza kwa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo, na hivyo kuwataka wananchi kuitumia fursa hiyo kuboresha maisha yao.

Aidha, Dkt. Biteko amesema ana deni kwa wananchi la kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, akiahidi kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wake kikamilifu, akitoa wito wa umoja na ushirikiano miongoni mwa wananchi, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mshikamano na kujitoa kwa pamoja. 

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.