Na Ibrahim Rojala - Geita.
Taasisi za kifedha nchini zimetakiwa kufanya maamuzi magumu, pasipo kuathiri sheria za taasisi za kifedha na kuja na mipango maalum itakayowahusu wachimbaji wadogo wa madini ambao mara nyingi wamekuwa wakikopeshana fedha wao kwa wao katika utekelezaji wa shughuli zao za kiuchumi katika sekta ya madini.
Rai hiyo imetolewa Mei 9, 2026 na Waziri wa Madini, Antony Mavunde wakati akizindua tawi la Benki ya Exim mkoa wa Geita ambapo amebainisha kuwa wachimbaji wadogo wa madini ni kundi ambalo limekuwa na mchango wa asilimia 40 katika kiasi cha shilingi trilioni 1.2 ambazo hukusanywa na kuingizwa katika mfuko mkuu wa serikali kupitia sekta ya madini.

Waziri Mavunde pia ameleeza kwamba mchango wa mkoa wa Geita katika pato la Taifa kupitia sekta ya Madini ni mkubwa na kwa mwaka huu wa fedha mkoa wa Geita umeongoza baada ya kuvuka lengo la ukusanyaji wa kiasi cha shilingi bilioni 327 na kuvuka lengo hilo kwa kukusanya bilioni 378, kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha kwenye masoko na vituo vya ununuzi wa madini yote ikiwa ni kutokana na mazingira mazuri ya ufanyikaji wa biashara ya madini nchini.
"Kwanini Exim mmekuja hapa hamjaenda sehemu nyingine,iko sababu iliyowaleta Geita,wanasema tone la asali linavutia nzi wengi kuliko dumu la pombe, Geita ni tone la asali kwasababu ya kazi nzuri ambayo imefanywa na uongozi wa Dkt. Samia Suhulu Hassan kwenye sekta ya madini,"

"Hivi sasa sekta hii inakua kwa kiasi na mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa umefikia aslimia 10.1,sio jambo dogo, pato letu la Taifa ni shilingi trilioni 220, sekta ya Madini peke yake tunachangia trilioni 20," amesema Waziri Mavunde.
Akizungumzia uzinduzi wa tawi hilo, Afisa Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu ameeleza kuwa imekuwa ni siku ya kihistoria inayoendana na uimarishaji wa ahadi ya taasisi hiyo ya kifedha kwenda pale ambapo uchumi unakua na kuwa karibu na watu wanaojenga uchumi huo kila siku.

Aidha, Matundu ameeleza kwamba benki hiyo inatambua umuhimu wa sekta ya madini ambayo ni nguzo kuu ya uchumi kwa mkoa wa Geita na mchango mkubwa kwa Taifa na benki hiyo inachochea sekta hiyo kwa kutoa mikopo, kusimamia miamala ya biashara na kuwezesha uwekezaji.
"Zaidi ya uzinduzi huu,leo tunaimarisha ahadi yetu ya kuwa benki inayokwenda pale ambapo uchumi unakua na kuwa karibu na watu wanaoujenga uchumi huo kila siku"amesema

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashim Komba ameishukuru Exim Bank kwa mchango wa vifaa kwaajili ya watoto njiti katika hospitali ya Manispaa ya Geita alivyoeleza kuwa vimesaidia kuongeza chuchu ya utoaji wa huduma kwa watoto walio katika kundi hilo.
"Wadau wetu hawa wa Exim Bank waligusa maisha ya watoto wadogo pamoja na akina mama katika hospitali ya Manispaa ya Geita, ukienda pale hospitali ya Manispaa ya Geita, Dokta Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa sana wa kuchochea ukuaji wa sekta ya afya kwenye maeneo yetu,"

"Lakini wenzetu wa Exim Bank wamekuja kuongeza chachu ya utoaji wa huduma, wamekuja kuongeza uhakika wa tabasamu kwa wananchi, wametukabidhi vifaa kwaajili ya wodi ya watoto wadogo kabisa," amesema DC Komba.
Discussion
Reader comments
0 contributions